Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Zaidi ya kilo 200 za Madawa ya Kulevya zateketezwa
13 Nov, 2020
Zaidi ya kilo 200 za Madawa ya Kulevya zateketezwa

Mhe. Jaji Edwin Kakolaki wa Mahakama Kuu akishirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga, pamoja na taasisi nyingine ikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, NEMC na Mawakili wa kujitegemea, leo wamefanya zoezi la uteketezaji wa madawa ya kulevya jijini Dar es salaam.

Mhe. Jaji Edwin Kakolaki ameeleza kuwa "Kiutaratibu baada ya kesi kuwa zimekwisha kusikilizwa mahakamani na kuisha, mahakama baada ya kuwa imepokea kile kielelezo, huwa ni kielelezo cha mahakama na hivyo baadae hutoa amri ya kwamba kielelezo hicho kiteketezwe"

Pia aliendelea kueleza kuwa zoezi hilo hufanyika kwa uwazi ili kuwawezesha watanzania kufahamu ya kuwa kesi inapofika mahakamani ni lazima kile kielelezo kiteketezwe baada ya kesi kufanyiwa kazi.

Nae Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga ameeleza kuwa jumla ya madawa ya kulevya yaliyoteketezwa leo ni kilo 119.074 aina ya Heroin, kilo 3.93 aina ya Kokein na Kilo 120 aina ya Bangi, ambapo zimetokana na kesi mbalimbali 15, ukilinganisha na mwaka jana jumla ya kesi zilizoteketezwa zilikuwa 17 kwa mkoa wa Dar es salaam peke yake.

"Na kesi ambayo ilikuwa ina heroin nyingi ni kesi ambayo ilikuwa inahusisha Wapakistani ambao walikuwa 12 na wamefungwa miaka 30 jela ijumaa iliyopita"

Mkurugenzi wa Mashtaka aliendelea kueleza kuwa waliamua kuachana na utaratibu wa kutoa thamani ya madawa ya kulevya yaliyokamatwa na kuteketezwa ili kuepusha ushawishi wa watu kujihusisha katika biashara hiyo haramu.

Aidha, Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bi. Bertha Mamuya amesema kuwa moja ya madhara ya madawa ya kulevya ni pamoja na kuharibikiwa akili, kupoteza nguvu kazi na kuwa tegemezi katika jamii inayokuzunguka, na pia Serikali hutumia gharama kubwa za matibabu.