WANAWAKE WA NPS MAKAO MAKUU NA MKOA WA DODOMA WATEMBELEA MAKAO YA TAIFA YA WATOTO KIKOMBO
Kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma walifanya matendo ya huruma kwa kuwatembelea watoto wenye uhitaji maalum na kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo.
Msaada huo ulikabidhiwa tarehe 7 Machi, 2026 ambapo wanawake hao walitoa mahitaji mbalimbali muhimu kwa ajili ya watoto hao, yakiwemo taulo za kike, sabuni za kufulia, viatu, mafuta ya kupikia, mchele, maharage, jola la vitambaa kwa ajili ya sare za shule, vifaa vya shule, mihogo, katoni za juisi, biskuti, masanduku ya chuma pamoja na fedha taslimu. Msaada huo umelenga kusaidia kuboresha mahitaji ya msingi ya watoto wanaoishi katika makao hayo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, wawakilishi wa wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka walisema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa vitendo, kwa kuonesha upendo, huruma na mshikamano kwa watoto wanaoishi katika mazingira yenye changamoto mbalimbali.
Aidha, wanawake hao walieleza kuwa lengo la kufanya matendo hayo ya huruma ni kuwafariji na kuwapa matumaini watoto hao pamoja na kuhamasisha jamii kuendelea kuwajali watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ili wajisikie kuwa sehemu ya jamii na kupata fursa bora za maendeleo ya maisha yao.
