NPS YASUKA MIPANGO MIPYA MWAKA WA FEDHA 2026/27
Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekutana na kufanya kikao kazi kwa lengo la kuweka mikakati mipya ya mwaka wa fedha wa 2026/2027 ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Julai 16, 2026 Jijini Arusha Mkurugenzi wa Mashitaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema kuwa kikao hicho kimejikita kujadili utekelezaji wa majukumu ya taasisi, kuweka mikakati ya mwaka mpya wa fedha na kuimarisha utendaji kwa kuzingatia uwajibikaji, ubunifu na matokeo.
Amesema kuwa kuanza kwa mwaka mpya wa fedha kunapaswa kwenda sambamba na mipango madhubuti ya utekelezaji wa shughuli kwa kuzingatia Mpango wa Muda wa Kati wa Matumizi ya Serikali (MTEF), huku kila kiongozi akihakikisha malengo yaliyowekwa yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Aidha, amewahimiza viongozi kufanya kazi kwa bidii, kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa shughuli katika ngazi za mikoa na wilaya ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na Ofisi zinaendelea kuwa bora na zenye matokeo chanya.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mashtaka amesisitiza umuhimu wa kuandaa taarifa za utendaji kwa umakini na kwa ubora wa hali ya juu, akieleza kuwa taarifa hizo ni nyenzo muhimu za kupima mafanikio ya taasisi na ni kumbukumbu rasmi zinazotumika katika maamuzi na mipango ya maendeleo ya Ofisi.
Pia amewataka Wakuu wa Divisheni na Vitengo kuhakikisha wanawawezesha watumishi walio chini yao kwa kuwapatia ujuzi unaohitajika, vitendea kazi stahiki pamoja na usimamizi na mwongozo unaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
