NAIBU DPP AWAHIMIZA WATUMISHI KUFANYA MAZOEZI KUBORESHA AFYA NA UTENDAJI KAZI
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bibiana Kileo, amewahimiza watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kushiriki kikamilifu katika shughuli za michezo na mazoezi ili kuimarisha afya zao, mshikamano pamoja na kuboresha utendaji kazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza la michezo la ofisi hiyo lililofanyika tarehe 28 Februari, 2026 katika viwanja vya Viwanja vya Kilimani jijini Dodoma, Bi. Kileo alisema michezo ni njia muhimu ya kuwajenga watumishi kiafya na kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kila siku.
Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, riadha, mpira wa kikapu, kuvuta kamba, kukimbia na yai kwenye kijiko, shindano la kunywa soda, kukimbiza kuku na kukimbia ndani ya gunia.
Katika tukio hilo, watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka waliungana na wenzao kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo pamoja na kujenga afya za watumishi.
Bi. Kileo alisema kufanyika kwa bonanza hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amezihimiza wizara na taasisi za serikali kuimarisha michezo kwa watumishi ili kuboresha afya na kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza kama presha na kisukari.
“Tunafanya mabonanza haya kwa kutii maelekezo ya Mkuu wa Nchi na kwa dhamira ya dhati ya taasisi yetu iliyo chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, ili kuimarisha afya za watumishi na kuhakikisha tunaboresha utendaji kazi wetu,” alisema Bi. Kileo.
Aidha, aliwataka wawakilishi wa Mashtaka Sports Club kutoka mikoa mbalimbali walioshiriki katika bonanza hilo kwenda kuwahamasisha watumishi wenzao kuendelea kufanya mabonanza kila mwisho wa mwezi ili kuimarisha afya zao. Alisema menejimenti ya ofisi hiyo ina dhamira ya kuendelea kuyaunga mkono mabonanza hayo.
Alifafanua kuwa katika Mkutano Mkuu wa watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka uliofanyika jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Mashtaka alielekeza kuwa ofisi zote za mashtaka nchini ziwe zinaandaa mabonanza ya michezo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa lengo la kuimarisha afya za watumishi na kuendelea kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Sambamba na hilo, Bi. Kileo aliwashukuru watumishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushiriki katika bonanza hilo na kusisitiza kuwa matukio kama hayo yanasaidia kuimarisha mahusiano mazuri, umoja na mshikamano kati ya taasisi hizo.
Aidha, alipendekeza kuandaliwa kwa kalenda ya pamoja ya michezo ili kuwezesha taasisi hizo kukutana mara kwa mara katika matukio ya michezo ndani ya mwaka.
