"Zaidi ya asilimia 90 ya makosa ya jinai yanayofanyika nyuma yake kuna msukumo wa kupata kipato." Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema yapo makosa machache ambayo wakiamua kuyachunguza hayahusiani na kipato au fedha lakini asilimia 90 ya makosa mengi nyuma yake kuna msukumo wa kujipatia fedha.
"Tumekuwa tukipeleleza na kuendesha mashtaka kwa makosa husika tu lakini tumekuwa hatutafuti fedha ambazo zimekuwa na ushawishi mkubwa wa kufanya uhalifu huo." Mkurugenzi Mwakitalu amebainisha hayo wakati akifungua Mafunzo kwa Wapelelezi na Wachunguzi yahusuyo Makosa ya Uhalifu wa Kifedha yaliofanyika tarehe 2 Septemba, 2024 Jijini Dar es salaam.
Sambamba na hilo DPP amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kwasababu yatawasaidia kudhibiti eneo hilo na kukatisha tamaa ya wahalifu wengi na kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa.
"Tulikuwa na wabobezi wachache sana katika maeneo haya ambao unaweza kuwataja kwa majina lakini kwa kutengeneza timu hii ya wabobezi 25 kwa kuanzia, tunaamini sasa tunaweza kukabiliana na uhalifu huu kwa kiasi kikubwa." Amefafanua hayo Mkurugenzi wa Mashtaka Mwakitalu.
Aidha, DPP amewataka washiriki hao kuwekeza nguvu na akili katika mafunzo hayo ili waweze kukipata kile walichokikusudia.
"Tunawategemea kama taifa kwa kiasi kikubwa sana na tunaamini baada ya kutoka hapa tutapata kundi lingine kubwa la wakufunzi ambao wataenda kuhamisha ujuzi huu kwa watendaji wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mahali hapa." Amebainisha hayo Mkurugenzi Mwakitalu.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bibiana Kileo ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuongeza utaalamu zaidi wa kuchunguza na kupeleleza juu ya makosa ya uhalifu wa kifedha.
Naibu Mkurugenzi amefafanua kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamegawanyika katika makundi matatu ambao kundi la kwanza na la pili ni Wapelelezi na Wachunguzi ambao wapo katika Kituo Jumuishi kinachoshughulika na Uhalifu wa Kifedha Tanzania Bara (ECC) na Zanzibar (ZECC) na kundi la tatu ni wajumbe wachache ambao hawafanyi kazi moja kwa moja na Kituo Jumuishi kinachohusika na Makosa ya Uhalifu wa kifedha (ECC).
Aidha Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amewataka washiriki wote waliopata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo kuweka umakini zaidi kwani matarajio yao makubwa katika mafunzo hayo sio tu kulenga kusaidia taasisi za Haki Jinai bali kuleta tija kwa taifa lote na kupeleka ujumbe ndani na nje ya nchi kwamba uhalifu haulipi.