Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

WAZIRI SIMBACHAWENE ASISITIZA JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA TEHAMA KATIKA TAASISI ZA UMMA
06 Sep, 2023
WAZIRI SIMBACHAWENE ASISITIZA JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA TEHAMA KATIKA TAASISI ZA UMMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amezitaka Taasisi zote za  Serikali kujikita katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi wa Taasisi unaosaidia kutatua changamoto za kiutendaji.

Waziri Simbachawene amezungumza hayo wakati akihutubia kwenye Hafla ya Makabidhiano ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya, Kuchakata na Kutunza Kumbukumbu za Kesi za Jinai (Case Management Information System) na Tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iliyofanyika tarehe 23 Agosti, 2023 Makao Makuu Jijini Dodoma.

Mhe. Waziri ameeleza kuwa Mfumo huo ambao umejengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka utakuwa ni mwarobaini katika kuhakikisha kwamba usimamizi wa mtiririko wa kesi unakwenda vizuri na haki ya mtu inapatikana kwa wakati.

"Nimejulishwa kuwa hadi sasa zaidi ya kesi 17,411 zimesajiliwa katika mfumo huu ambapo kati ya kesi hizo kesi 7,361 zimeshafikia mwisho na kutolewa hukumu. Na baadhi ya kesi 10,050 zipo katika hatua mbalimbali za maamuzi. Hakika hayo ni mafanikio na maendeleo makubwa katika nchi yetu ambayo yamelenga kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na pia ni mfano wa kuigwa kwa Taasisi nyingine zinazohusika na utoaji wa huduma kwa umma." Ameyasema hayo Mhe. Waziri.

Waziri Simbachawene ameendelea kueleza kuwa lengo kuu la Mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kushughulikia usimamizi na uendeshaji wa kesi za jinai. Na kwa ujumla mfumo huo utakuwa wazi na kupunguza malalamiko kwa wananchi juu ya maamuzi mbalimbali yanayotolewa na mahakama.

Sambamba na hilo Mhe. Simbachawene amesema kuwa Tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imejengwa kwa lengo la kusaidia utoaji wa taarifa sahihi kwa wananchi na wadau zinazohusiana na shughuli mbalimbali za Ofisi ya Taifa ya Mashtaka

Pia Waziri Simbachawene alitoa wito kwa Taasisi nyingine za umma katika kuhakikisha kwamba hazisuisui na zinafanya jitihada kuongeza matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao kama jinsi sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 inavyoeleza.

"Hii itaongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na pia kutimiza azma kwa Serikali ya awamu ya sita ya  Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akisisitiza sana kwa nia ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema wao kama Serikali dhamira yao ni kuona haki zote zinatolewa kwa wakati, hivyo ana imani mfumo huo utakuwa chachu ya kufanikisha hilo.

"Haki ni suala muhimu sana na inapaswa itolewe kwa wakati na hivyo kupitia mifumo ya TEHAMA tunataka kuhakikisha haki zinatolewa kwa wakati". amesema Waziri Gekul.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema kuwa Mfumo huo ni nyenzo muhimu sana ambayo itasaidia katika kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwani kupitia Mfumo huo utasaidia kutunza Kumbukumbu za majalada yote wanayopokea kutoka Vyombo vya Uchunguzi hadi yanapohitimishwa Mahakamani.

"Kupitia Mfumo huu haki za mashtaka zitapandishwa, hukumu zitapatikana humu, na pia hata mtiririko wa mgawanyo wa majalada utaonekana katika mfumo huu."  Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.