Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

WAZIRI PINDI CHANA AFANYA ZIARA KATIKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA
03 Nov, 2023
WAZIRI PINDI CHANA AFANYA ZIARA KATIKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefanya ziara ya kutembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kujadililiana mambo mbalimbali yahusuyo utendaji kazi wao, Muono wa mbele, mafanikio na changamoto wanazokutana nazo.

Ziara hiyo imefanyika tarehe 2 Novemba, 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo Waziri Pindi Chana ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa majukumu wanayoyafanya katika kushughulikia mashauri mbalimbali ya Jinai kwani kesi nyingi zimefanikiwa kuendeshwa vizuri Mahakamani.

"Dhamana tuliyopewa ni kuhakikisha Haki, Amani na Usalama vinapatikana katika nchi yetu." Ameyasema hayo Mhe. Waziri. 

 Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja Ofisi hiyo ilipata mafanikio katika kuendesha Mashtaka ambayo ni kuokoa fedha zilizopatikana kwa njia ya Uhalifu na kutaifisha mali zilizotumika kwenye Uhalifu huo ili kuhakikisha wahalifu hawanufaiki chochote na Uhalifu.

"Hivyo basi katika kipindi hicho tumeweza kuokoa fedha, magari, nyumba, viwanja na madini kutoka kwa wahalifu ikiwa ni lengo kuwakatisha tamaa wahalifu ili watambue kuwa uhalifu haulipi." Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu. 

Aidha, katika taarifa hiyo Mkurugenzi Mwakitalu amesema kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanikiwa kupunguza mlundikano wa mahabusu na wafungwa katika magereza zilizopo nchini kwani katika miezi michache iliyopita mahabusu walikuwa ni wengi kuliko wafungwa. Kwa taarifa za magereza kwa mwezi Oktoba mahabusu waliopo ni jumla ya 9,000 na wafungwa waliopo ni jumla ya 18,000. Na hii ni moja ya sababu ya uimarishaji wa ofisi za Mashtaka Mikoa pamoja na kusogeza huduma katika ofisi za Mashtaka Wilaya kwani imewezesha mashauri mengi kusikilizwa kwa wakati na kwa haraka na hivyo kupelekea haki za washtakiwa kupatikana kwa haraka.

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Mashtaka ameeleza baadhi ya changamoto zinazoikabili Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni pamoja na Ufinyu wa Bajeti, uhaba wa watumishi, upungufu wa vitendea kazi, ongezeko la aina mpya ya Uhalifu kwasababu makosa mengi yanafanyika kwa njia ya mitandao hivyo basi ili kuweza kudhibiti uhalifu huo  Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wapelelezi na wadau wengine wa haki jinai wanapaswa kujengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ili kuweza kukabiliana na changamoto hiyo.

Nae pia Mkurugenzi wa Divisheni ya Utaifishaji Mali, Makosa yanayovuka Mipaka na Uhalifu Mahususi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Faraja Nchimbi alitoa shukrani kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kwa niaba ya Menejimenti na Watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kuahidi kuwa maelekezo ambayo yametolewa hususani katika  kuzingatia kwamba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iwekeze katika kufanya kazi kwa ukaribu na wadau kutoka ndani na nje ya nchi. Kuwekeza katika mikakati ya upatikanaji wa viwanja kwa maeneo ya makazi kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, kuongeza nguvu katika eneo la usimamiaji wa Utaifishaji na Urejeshaji Mali  zinazotokana na Uhalifu pamoja na maeneo mengine yanayopaswa kuboreshwa.

"Tunashukuru kwa pongezi ambazo umetoa na hii inaashiria namna ambavyo unatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni moja ya Taasisi zinazounda jumla ya Wizara ya Katiba na Sheria, na sisi tunaahidi kuyatekeleza na kuongeza ufanisi na utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kwamba kero zinazowakabili wananchi katika sehemu ya usimamizi wa Haki jinai zinaondoshwa." Amebainisha hayo Mkurugenzi Nchimbi.