Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

WAZIRI CHANA AZINDUA MIONGOZO MITATU (3) KUTOKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA
29 Sep, 2023
WAZIRI CHANA AZINDUA MIONGOZO MITATU (3) KUTOKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefanya Uzinduzi wa Miongozo Mitatu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambayo ni Kuwajali na kuwalinda Mashahidi, Urejeshaji na Utaifishaji Mali zinazotokana na Uhalifu pamoja na Ushirikiano wa Kisheria katika Masuala ya Jinai. 

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 27 Septemba, 2023 Jijini Dar es salaam ikiwa na lengo la kusaidia kuleta ufanisi na kuwezesha kujenga mfumo imara wa Kisheria katika upatikanaji wa Haki Jinai utakaowawezesha Wananchi kufanya shughuli zao kwa amani, utulivu na usawa.

Waziri Chana amesema kuwa Miongozo hii inatija kubwa kwa mashahidi ambao ndio nguzo muhimu katika upatikanaji wa Haki Jinai nchini kwani ili kuleta amani katika nchi na kutenda haki panahitajika kuwa na mashahidi.

Pia Dkt. Pindi Chana alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini kwani uamuzi huo unalenga kuhakikisha kuwa mapendekezo yaliyotolewa yatasaidia kuboresha mfumo wa Haki Jinai kwa kusaidia wananchi wengi kupata haki zao ikiwemo ulinzi wa mashahidi.

Aidha Waziri Chana ametoa wito kwa wananchi kuwa mabalozi wa amani kwa kutoa ushirikiano wa kutosha pale ambapo wanaona kuna uhalifu umefanyika au unafanyika wasiache kutoa taarifa katika vyombo husika.

"Ikiwa kama kuna eneo mtu kwa namna moja ama nyingine au kikundi cha watu watakuwa wanatenda uhalifu, sisi kama Wizara tutakuwa tayari kuwapokea kama wateja wetu halali. Tunahitaji Tanzania iwe ni mfano wa kuigwa na Mataifa mbalimbali kwani Tanzania sio sehemu salama ya Makosa ya Jinai." Ameyasema hayo Waziri Chana.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema kuwa wana imani Miongozo hiyo itaenda kuwaongezea tija katika utendaji wao wa kazi za kila siku.

Pia Mkurugenzi Mwakitalu alitoa shukrani kwa Wadau mbalimbali, Wasimamizi wa Sheria na Vyombo vya Uchunguzi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kuandaa nyaraka za Miongozo hiyo.

"Kwa kushirikiana na Taasisi hizi tumeweza kuelewa maeneo ambayo yana mapungufu katika utendaji kazi wetu kwa kufahamu changamoto pamoja na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuweka katika Miongozo yetu." Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Sambamba na hilo Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa kupitia miongozo hiyo itasaidia kuwa na usimamizi unaofanana katika kushughulikia Mashauri ya Jinai kutoka sehemu mbalimbali na pia itasaidia kuhakikisha wahalifu hawanufaiki na mali wanazopata kwa njia ya uhalifu, au mali zinazotumika katika kutenda uhalifu.