WATUMISHI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA WASHIRIKI KWENYE MAADHIMISHO YA MEI MOSI, 2025 MKOANI SINGIDA

Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka Makao Makuu Jijini Dodoma, Mkoa wa Singida,Dodoma na Manyara pamoja na wawakilishi wa TUGHE kutoka baadhi ya mikoa wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu, wameungana na Wafanyakazi wengine nchini kuadhimisha siku ya Wafanyakazi Duniani (MeiMosi) ambapo Kitaifa imeadhimishwa tarehe 01 Mei, 2025 kwenye viwanja vya Bombadia Mkoani Singida.
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho haya yaliyoandaliwa na Shirikisho la vyama 13 vya Wafanyakazi (TUCTA) ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi nchini, serikali imefanya maamuzi ya kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1.
"Ninayo furaha ya kuwatangazia kwamba, katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu, Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1, nyongeza hii itakayoanza kutumika mwezi Julai, 2025 itaongeza mshahara wa kima cha chini kutoka Shilingi 370,000/= hadi Shilingi 500,000/=. Ngazi nyingine za mshahara nazo zitapanda kwa viwango tofauti tofauti kulingana na uwezo wa kibajeti." Amefafanua Rais Dkt. Samia.
Aidha, maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo "Uchaguzi Mkuu 2025, Utuletee viongozi wanaojali haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote tushiriki."