Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Washtakiwa 57 waachiwa huru katika gereza la Shinyanga
02 Sep, 2020
Washtakiwa 57 waachiwa huru katika gereza la Shinyanga

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga mnamo tarehe 31 Agosti, 2020 aliwaachia huru washtakiwa 57, wakiwepo wanaume 47 na wanawake 10 waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbalimbali ambao waliokuwa wamewekwa katika gereza la Shinyanga.

Bw. Biswalo Mganga aliendesha zoezi hilo wakati alipotembelea gereza la Shinyanga akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wizara ya Katiba na Sheria.

Akizungumza katika tukio hilo Bw. Amon Mpanju alisema wametembelea gereza la Shinyanga wakiwa ni wadau katika mfumo wa upatikanaji haki ili kwa pamoja kuweza kuwasikiliza na kufahamu changamoto za kwenye magereza ili kuzitafutia suluhisho.

Akizungumza wakati akiwaachia huru mahabusu hao Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga aliwataka mahabusu hao waliochiwa huru kuhakikisha hawarudii makosa waliyoyafanya kwa kuwa anahitaji nchi yenye amani na aliwaeleza wazi kuwa yeyote kati yao ambae anajua hawezi kwenda kutulia na kuwa raia mwema abaki gerezani.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju aliwasihi mahabusu hao walioachiwa huru wakirudi uraiani kwenda kuwa raia wema na wale waliobakia kukaa kwa amani na kuwasikiliza walezi wao gerezani huku wakifundishana wao kwa wao kutenda mema.

Awali kabla ya kuanza ziara ya kutembelea gereza hilo la Shinyanga wajumbe walipata nafasi ya kumtembelea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainabu Telack na kuzungumza nae juu ya ziara hiyo ambapo alipongeza juu ya hatua hiyo na kueleza kuwa ziara kama hizo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali za magerezani.

Wakati wa ziara hiyo ya kutembelea magereza wajumbe walichangia kiasi cha shilingi laki tatu (300,000/=)ambazo walizitoa kwa lengo la kuliwezesha gereza hilo kununua cherehani, sabuni na ving’amuzi kufuatia ombi la wafungwa hao.