Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

WASHITAKIWA 16 WA UJANGILI WAFUNGWA MIAKA 20 HADI 30 KWA KUKUTWA HIFADHINI NA NYARA ZA SERIKALI.
29 Nov, 2020
WASHITAKIWA 16 WA UJANGILI WAFUNGWA MIAKA 20 HADI 30 KWA KUKUTWA HIFADHINI NA NYARA ZA SERIKALI.

Washitakiwa 16 katika kesi Namba 8 wametiwa hatiani kwa makosa ya ujangili na kuhukumiwa jumla ya kifungo kati ya miaka 20 hadi 30 jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Serengeti.

washitakiwa hao walikamatwa mwaka 2019 kwa nyakati tofauti ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mapori ya Akiba ya Ikorongo, Grumeti na Hifadhi ya Jamii ya Ikona na kushitakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kuingia,kupatikana na silaha za jadi na kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Washitakiwa hao kwa nyakati na sehemu mbalimbali walikamatwa na nyara tofauti ikiwemo vipande vya nyama za Pundamilia, Impala, Nyumbu na Kongoni zenye jumla ya thamani ya Shilingi Milioni 29 na laki 9 na Elfu 55 (29,955,000).

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Serengeti Ismael Ngaile amesema kuwa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ambayo inatoa adhabu ya isiyozidi miaka 30 na isiyopungua miaka 20 .

Washitakiwa hao ni Makena Mwita (21) Mkazi wa Mbirikiri , Rubeni Mwita (28) wa Bonchugu ambao kila mmoja amehukumiwa miaka 30 jela huku Mugendi Ng’ombe (51) mkazi wa Nyichoka,Richard Nyambaya(35)na Mussa Masese(42)wakazi wa kijiji cha Nyamatoke walihukumiwa kila mmoja miaka 25

Aidha Manungu Makoye na Mazoya Daddi ambao wamehukumiwa miaka 20, na wenzao Simion Nyamhanga(28)mkazi wa Nyamakendo,Benard Gambachera(50)mkazi wa Robanda, Marwa Chacha (30) Marwa Mtatiro(19)Mnanka Bisare(28)Sarya Matiko(20) Maduhu Mila(35)mkazi wa kijiji cha Singisi,Bhoke Mwita(53)na Juma Masyora(43)wakazi wa Bisasara.

Mapema waendesha Mashitaka wa serikali Josephat Emmanuel, Abeid Nnko na Jakobo Matatala mbele ya Hakimu Ngaile waliomba Mahakama kutoa adhabu kali katika kesi hizo za Uhujumu uchumi kwa kuwa vitendo vya ujangili vinazidi kushamiri na kuathiri maliasili za Nchi, huku baadhi ya washitakiwa wakishindwa kujitetea.