Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

WANAWAKE KUTOKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA WASHIRIKI KUFANYA MATENDO YA HURUMA.
07 Mar, 2024
WANAWAKE KUTOKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA WASHIRIKI KUFANYA MATENDO YA HURUMA.

Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika tarehe 8 Machi, 2024 wanawake kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  Makao Makuu Jijini Dodoma wameshiriki kwa pamoja kutoa Misaada mbalimbali kwenye Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. 

Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo  Hospitalini hapo leo tarehe 6 Machi, 2024 Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bi. Chivanenda Luwongo amesema wanawake kutoka Idara na Vitengo mbalimbali vya Ofisi ya taifa ya Mashtaka, wamechangishana fedha ambazo wamezitumia kununulia mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kuwapa msaada wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali hiyo ya Rufaa.

Bi. Luwongo amesema kuwa wametoa matibabu kwa wagonjwa wanaume 3 na wanawake 2 waliolazwa kwa muda mrefu ambapo watagharimia matibabu yao kwa muda wa siku 7 kwa kuwapa Dawa, Gharama za mtoto mmoja anayefanyiwa upasuaji pamoja na dawa za siku tatu pamoja na wagonjwa wenye mahitaji maalumu.

Ametaja misaada mingine  kuwa ni pamoja na Sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kupaka, Asali kwa ajili ya wagonjwa wenye majeraha na Maziwa kwa ajili ya watoto wadogo wanaotibiwa na kuhudumiwa hospitalini hapo bila kuwa na wazazi.

Kwa upande wake Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Bw.  Stanley Mahundo ameishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuchagua Hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa misaada mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia  wanawake na watoto wanaougua maradhi mbalimbali huku akiahidi misaada hiyo kuwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa. 

“Baadhi ya wanawake na watoto hawana ndugu wa kuwahudumia ambao wanapata matibabu hapa hivyo kwa wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoa misaada hii mmefanya jambo la muhimu kwani misaada hii itawasadia kwa kiwango kikubwa." Amebainisha hayo Muuguzi Mfawidhi. 

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatafanyika Kitaifa tarehe 8 Machi, 2024 katika Wilaya ya  Chamwino, Makao Makuu Jijini Dodoma.