Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

DPP AWAPONGEZA MAWAKILI WA SERIKALI KWA KUFIKIA ASILIMIA 88 YA USHINDI WA MASHAURI
16 Jul, 2026
DPP AWAPONGEZA MAWAKILI WA SERIKALI KWA KUFIKIA ASILIMIA 88 YA USHINDI WA MASHAURI

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, amewapongeza Menejimenti na Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa kuendelea kuimarisha utendaji kazi uliowezesha Ofisi kufikia kiwango cha asilimia 88 ya ushindi wa mashauri.

DPP Mwakitalu alitoa pongezi hizo wakati akifungua Kikao Kazi cha Mkurugenzi wa Mashtaka, Menejimenti na Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kilichofanyika tarehe 15 Julai, 2026, Jijini Arusha. Alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi, weledi, uaminifu na kujituma kwa Mawakili wa Serikali, sambamba na ushirikiano mzuri na wadau mbalimbali wa mnyororo wa haki jinai.

Alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Ofisi, kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya mashtaka na kuweka mikakati ya pamoja ya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, alisema kikao hicho kitatoa fursa kwa washiriki kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza na kuandaa mikakati madhubuti ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Katika hotuba yake, DPP Mwakitalu alisema Mawakili wa Serikali ni nguzo muhimu katika mfumo wa haki jinai, kwani kiwango cha imani ya wananchi katika utoaji wa haki kinategemea namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kutumia ipasavyo ushahidi unaowasilishwa na vyombo vya uchunguzi.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya Ofisi hayawezi kupatikana kwa kufanya kazi kwa kujitegemea, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu na wadau wote wa mnyororo wa haki jinai, wakiwemo Jeshi la Polisi, Mahakama, taasisi za uchunguzi na wadau wengine wanaoshiriki katika utekelezaji wa haki.

DPP Mwakitalu pia aliwahimiza Mawakili wa Serikali kuendelea kujifunza na kujijengea uwezo ili kuendana na mabadiliko ya sheria, Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia pamoja na mbinu mpya za uchunguzi na uendeshaji wa mashauri.

Akihitimisha hotuba yake, aliwataka washiriki watakaporejea katika vituo vyao vya kazi kuendeleza utamaduni wa kujisomea sheria, hukumu, machapisho ya kitaaluma na nyenzo nyingine za kisheria ili kuongeza umahiri wao, kuimarisha ubora wa huduma na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu ya mashtaka.