Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Waliohusika na kifo cha Dokta Mvungi wahukumiwa kunyongwa hadi kufa
18 Sep, 2020
Waliohusika na kifo cha Dokta Mvungi wahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam tarehe 17/09/2020 katika kesi Na.54/2020 imewatia hatiani washtakiwa watano kati ya sita kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya Dokta Edmund Sengondo Adrian Mvungi. Washtakiwa hao ni Msigwa Matonya pamoja na wenzake watano.

Tukio hilo la mauaji lilitokea mnamo tarehe 3/11/2013 nyumbani kwake marehemu Dokta Mvungi maeneo ya Kibwegere Mbezi Msakuzi katika Wilaya ya Ubungo Mkoa wa Dar es salaam, ambako alivamiwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali hatarishi za mwili kwa kutumia vitu vyenye ncha kali ili kuweza kuiba Mali mbalimbali, jambo lililopelekea kifo chake akiwa kwenye matibabu huko Afrika Kusini.

Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Kulita ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Mashtaka ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Credo Rugaju, Lilian Lwetabura na Veronica Mtafya, ambapo katika kuthibitisha kosa hilo Jamhuri iliita mashahidi 16 na kuwasilisha jumla ya vielelezo 15.

Aidha Mahakama hiyo pia iliweza kumuachia huru mshtakiwa namba 5 ambaye ushiriki wake Mahakama imeona haukuthibitishwa ipasavyo pasipo kuacha shaka kama Sheria inavyotaka katika kesi za Jinai.