WAKUHUMIWA KUNYONGWA MPAKA KUFA KWA KOSA LA MAUAJI

Mahakama Kuu Kanda ya Manyara katika kikao kilichoketi Babati Mkoani Manyara imewahukumu Vita Boay (37) na January Seroneti (26) adhabu ya kunyongwa mpaka kufa baada ya kuwakuta na hatia kwa kosa la mauaji
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 30 Juni, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Ninelwa Mwihambi baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na Jamhuri.
Katika shauri la Jinai namba 3065/2025, Bw. Vita ambae ni mkazi wa Kijiji cha Maziriga-Nduguti wilaya ya Mkalama Mkoani Singida na Bw. January ambae ni mkazi wa kijiji Cha Maghang-Dongobesh ndani ya wilaya ya Mbulu mkoani Manyara walikuwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji kinyume na vifungu 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu , (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)
Washtakiwa walitenda kosa hilo tarehe 7 Julai, 2024 katika Kijiji Cha Dongobesh Wilaya ya Mbulu katika Mkoa wa Manyara, ambapo walimuua Gidion Paulo na kuchukua pikipiki yake. Pikipiki hiyo ilikutwa nyumbani kwa Mshtakiwa Bw. Vita Boay.
Kesi hiyo imeendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Manyara.