Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Wafungwa miaka ishirini (20) kwa kukutwa na Nyara za serikali
20 Aug, 2020
Wafungwa miaka ishirini (20) kwa kukutwa na Nyara za serikali

Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi kanda ya Bukoba mnamo tarehe 17/08/2020 mbele ya Mheshimiwa Jaji Lilian Mashaka kupitia shauri la Uhujumu Uchumi No.1/2020 la Jamhuri dhidi Paulo Andrea @Mbwilande na John Paulo imewakuta na hatia washtakiwa wote wawili kwa kosa la kukutwa na Nyara za serikali ambazo ni meno ya tembo vipande vitatu, sawa na tembo wawili yenye thamani ya dola za Kimarekani elfu 30 sawa na Tsh 68,382,000/=

Washtakiwa hawa walikamatwa na meno hayo ya Tembo na askari wa doria wa Maliasili mnamo tarehe 22/07/2018 katika kijiji cha Nyamigere Wilaya ya Biharamulo Mkoa wa Kagera.

Washtakiwa wamepewa adhabu ya kulipa faini Tsh. mil 683,820,000/= au kwenda jela miaka 20 kila mmoja. Washtakiwa wote wawili walishindwa kulipa faini hiyo na kupelekwa gereza la wilaya ya Bukoba kutumikia vifungo vyao. Mbali na adhabu hiyoya kifungo Mahakama ilitaifisha meno hayo ya tembo.

Katika hatua nyingine, tarehe 18/8/2020 Mahakama Kuu, kanda ya Bukoba mbele ya Mheshimiwa Jaji Lilian Mashaka kupitia shauri la Uhujumu Uchumi No.2/2020 la Jamhuri dhidi ya Jasson Pascal na Antidius Paschal imewakuta na hatia washtakiwa wote wawili kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali ambazo ni meno ya tembo na kuwapa adhabu ya kulipa faini Tsh. mil 337,800,000/= au kwenda jela miaka 20. Washtakiwa hawa walikamatwa na askari wa jeshi la polisi mnamo tarehe 4/04/2018 katika kijiji cha Bimulo wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera wakiwa na nyara hizo za serikali.

Mbali ya adhabu hiyo pia Mahakama imetoa amri ya kutaifisha meno hayo ya tembo na pikipiki moja yenye namba za usajili MC. 956 ATY aina ya GSM iliyokuwa inatumika kusafirisha nyara hizo. Washtakiwa wote wawili wameshindwa kulipa faini hizo na kupelekwa gereza la wilaya ya Bukoba kutumikia vifungo vyao.