Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Wafanyabiashara wawili wahukumiwa kulipa fidia ya shilingi bilioni 10.3
07 Sep, 2020
Wafanyabiashara wawili wahukumiwa kulipa fidia ya shilingi bilioni 10.3

Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita imewahukumu wafanyabiashara Bhawesh Chandular Gandecha na Ashvin Keshavbhai Patel raia wa Tanzania wenye asili ya kihindi kulipa fidia ya bilioni 10.3 na faini ya shilingi milioni 15 ambao walikutwa na hatia ya kusafirisha madini ya dhahabu ya Kg 93.26 kinyume na sheria yenye thamani ya bilioni 10.3 waliyosafirisha kupitia uwanja wa ndege wa Entebbe Uganda na kuyauza Falme za Kiarabu Dubai.

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la mawakili wa serikali mnamo Septemba 4, 2020, wakiongozwa na Paul Kadushi na Upendo Makondo, huku upande wa washtakiwa wakiwakilishwa na jopo la mawakili likiongozwa na Constantine Mutalemwa.

Hukumu hiyo ya kesi Na. 11 ya mwaka 2020 ya Uhujumu Uchumi imetolewa na Hakimu Mfawidhi Mwandamizi Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita Obadia Bogogwe baada ya watuhumiwa kukiri kusafirisha vipande Hamsini na mbili vya dhahabu vyenye uzito wa Kg 93.26.

Aidha Hakimu Bogogwe anasema tofauti na fidia hiyo watuhumiwa wametakiwa kulipa faini ya milioni 15 na endapo wangeshindwa basi wangetumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga alisema watuhumiwa wote wawili wamefanikiwa kulipa kiasi cha shilingi bilioni 7 papohapo na kuachiwa huru huku wakitakiwa kulipa bilioni 3 katika kipindi cha miezi sita, nje ya mahakama hiyo huku akiwaonya wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo vya Kuhujumu Uchumi kwa kutorosha madini kuachana na vitendo hivyo.