Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

UTATU YAIMARISHA USHIRIKIANO DHIDI YA UHALIFU
20 Nov, 2026
UTATU YAIMARISHA USHIRIKIANO DHIDI YA UHALIFU

Umoja wa Taasisi Zinazounda UTATU umekutanisha menejimenti zake ambazo ni ; Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Jeshi la Polisi kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu kwa kukabiliana na changamoto za kiuchunguzi na kimashtaka bila kukwamishwa na mipaka ya kiutendaji.

Kikao kazi hicho kimeanza leo, Novemba 18, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya Mkutano Mkuu wa Sita wa Taasisi Zinazounda UTATU unaofanyika kwa siku mbili hadi Novemba 19, 2026.

Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti wa UTATU ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, amesema ushirikiano wa taasisi wanachama umeimarisha ufanisi katika upelelezi, uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka. Akiongeza kuwa ushirikiano huo umechangia kukamilika kwa mashauri kwa wakati na kufikia kiwango cha ushindi wa kesi mahakamani cha asilimia 89 kwa mwezi Oktoba.
 
“Lengo la mkutano huu ni kutafuta suluhu za changamoto chache ambazo bado zinatukwamisha, kuweka mikakati ya pamoja na kufikia maazimio ya namna bora ya kushughulikia upelelezi, uchunguzi na uendeshaji wa kesi za jinai ili kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya uhalifu,” amesema Bw. Mwakitalu.

Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Ushirikiano wa Wadau Dhidi ya Uhalifu; Tanzania Salama Kuelekea Dira 2050”, unatarajiwa kufungwa Novemba 19, 2026, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari. Kupitia mkutano huo, taasisi wanachama zinalenga kufikia maazimio ya pamoja yatakayoimarisha mapambano dhidi ya uhalifu na utoaji wa haki kwa wakati.