Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MIFUMO YA KIDIJITALI IIMARISHWE KUBORESHA UTOAJI HAKI” – AG
20 Nov, 2026
MIFUMO YA KIDIJITALI IIMARISHWE KUBORESHA UTOAJI HAKI” – AG


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amezitaka taasisi zinazounda UTATU kuongeza matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji na usimamizi wa ushahidi pamoja na ufuatiliaji wa mashauri, akieleza kuwa mifumo ya kisasa na inayounganishwa itasaidia kuimarisha utendaji, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa haki jinai.

Akizungumza tarehe 19 Novemba 2026 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Taasisi zinazounda UTATU, Mhe. Johari amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuwa na mifumo ya kidijitali inayoweza kuwasiliana na kusomana, ili kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa, kufuatilia mwenendo wa utendaji na kusimamia mashauri kwa ufanisi zaidi.

“Ushahidi wa kidijitali unaweza kuongeza thamani na kuaminika kwenye vyombo vya maamuzi vya utoaji haki, hivyo, imarisheni ukusanyaji, uhifadhi na mnyororo wa utunzaji wa ushahidi,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, Mhe. Johari amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake ya kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini, akieleza kuwa juhudi hizo zimekuwa chachu ya kuboresha utendaji wa taasisi zinazohusika katika mnyororo wa haki jinai.

Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya upelelezi na uendeshaji wa mashtaka kwa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa taasisi husika akibainisha kuwa juhudi za pamoja zinazowekwa sasa zinaweza kuleta matokeo endelevu na manufaa kwa vizazi vijavyo.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kisheria na kushirikiana na taasisi hizo katika kutatua changamoto za kisheria zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Mkutano huo umewakutanisha wajumbe kutoka taasisi tano zinazounda UTATU, ambazo ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Jeshi la Polisi kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).