Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA WAMPELEKA JELA MIAKA 30
03 Jul, 2025
UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA WAMPELEKA JELA MIAKA 30

Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Mbeya imemuhukumu Siwema Simfukwe kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Hukumu hiyo imesomwa tarehe 30 June, 2025 na Hakimu Paul Rupia baada ya kuridhika na Ushahidi uliwasilishwa na upande wa Mashtaka.

Katika kesi hiyo Na. 28787 ya Mwaka 2024, Bw. Siwema ambaye ni mkazi wa Chitete iliyopo ndani ya Wilaya  ya Momba na Mkoa wa Songwe alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la Unyang`anyi wa kutumia Silaha Kinyume na Kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu,(Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022).

Mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 19 Agosti, 2024 katika maeneo Iwambi iliyopo ndani ya Wilaya na Mkoa wa Mbeya ambapo imethibitika kuwa mshtakiwa alimuibia mhanga simu aina ya Google Pixel 7 pro yenye thamani ya Tshs.1,050,000/=,  Simu ndogo ya Tecno yenye thamani ya Tshs. 45,000/= na kuiba kiasi cha fedha Tshs. 2,000,000/= kilichokuwa kwenye Account yake ya CRDB kwa njia ya Sim Banking kwenda kwenye namba ya mshtakiwa  na wakati anatenda tukio hilo alitumia silaha ambayo ni kisu kumtishia Mhanga uhai wake.

Siku ya tukio majira ya Saa mbili Usiku mhanga akiwa nyumbani kwake maeneo ya Iwambi yeye pamoja na watoto wake wawili walivamiwa na mshtakiwa nyumbani hapo akiwa ameshika kisu ambacho alitumia kumtishia Mhanga uhai wake kwa kutumia silaha hiyo na kufanikiwa kumuibia simu aina ya Google Pixel 7 pro yenye thamani ya Tshs.1,050,000/=, Simu ndogo ya Tecno yenye thamani ya Tshs. 45,000/= na kuiba kiasi cha fedha Tshs. 2,000,000/= kilichokuwa kwenye Account yake ya CRDB kwa njia ya Sim Banking kwenda kwenye namba ya mshtakiwa na kutoweka eneo la tukio.

Taarifa zilifikishwa katika Kituo cha Polisi Kati Mbeya tarehe 20 Agosti, 2024 na baada ya Jeshi la Polisi kufanya upelelezi wake walifanikisha kumkamata mshtakiwa tarehe 30 Agosti, 2024 maeneo ya kijiji cha Chitete ndani ya Wilaya  ya Momba na Mkoa wa Songwe akiwa na Silaha ambayo ni kisu alichotumia kutekelezea uhalifu na Simu ndogo ya Tecno mali ya mhanga.

Jumla ya mashahidi Kumi na moja (11) wa upande wa mashtaka  walitoa ushahidi na mtuhumiwa alijitetea mwenyewe.

Kesi hii imeendeshwa na mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mbeya.