Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

ULEGA AIPONGEZA NPS KWA KUIMARISHA ULINZI WA MTOTO
20 Nov, 2026
ULEGA AIPONGEZA NPS KWA KUIMARISHA ULINZI WA MTOTO

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa juhudi za kuimarisha ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili, hususan ukatili wa kijinsia na usafirishaji haramu wa binadamu, pamoja na kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.

Mhe. Ulega ametoa pongezi hizo Oktoba 13, 2026, alipotembelea Makao Makuu ya NPS, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Ulega amesisitiza umuhimu wa kuendesha mashauri ya watoto kwa haraka na ufanisi, akimpongeza Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, kwa mpango wa kuanzisha Kikosi Mahususi cha kushughulikia makosa dhidi ya watoto. Pia, ameahidi kushirikiana na wizara na taasisi husika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa pamoja.

“Hakuna jambo linaloniumiza na kunikera kama vitendo viovu vinavyotendwa dhidi ya watoto wetu. Kama kiongozi na mzazi, ninatamani kuona watoto wetu wanakua katika mazingira salama yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao,” amesema Mhe. Ulega.

Aidha, ameipongeza NPS kwa mpango wa kuanzisha kituo hicho, ambacho pamoja na uendeshaji wa mashauri na uratibu wa uchunguzi, kitafanya tafiti kuhusu vyanzo na viashiria vya ukatili dhidi ya watoto ili kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na vitendo hivyo. Vilevile, ameipongeza NPS kwa kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, hususan kupunguza msongamano katika mahabusu na magereza kwa kuzingatia sheria.

“Na mimi ninawaagiza kuendelea na utaratibu wa kufanya ukaguzi katika mahabusu na magereza mara kwa mara nchi nzima na kujiridhisha hakuna msongamano katika mahabusu hizo. Kesi zinazopaswa kwenda mahakamani ziende mahakamani na wale wanaopaswa kupewa dhamana kwa mujibu wa sheria wapewe dhamana,” amesema Mhe. Ulega. 


Akihitimisha hotuba yake amesema Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kuiunga mkono NPS katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za mashtaka na haki jinai nchini.