DPP AWATAKA VIONGOZI WA MASHTAKA KUSIMAMIA NIDHAMU NA UWAJIBIKAJI
Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester A. Mwakitalu, amewataka Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Wilaya pamoja na Waendesha Mashtaka Viongozi kusimamia kwa umakini nidhamu, uwajibikaji na weledi kwa watumishi walio chini yao, akisisitiza kuwa uongozi bora unaanza kwa kusimamia mienendo na utendaji wa watumishi.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha Mkurugenzi wa Mashtaka, Menejimenti, Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Wilaya pamoja na Waendesha Mashtaka Viongozi, kilichofanyika tarehe 20 Novemba, 2026 jijini Arusha, Bw. Mwakitalu amesema viongozi hao wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watumishi wanazingatia maadili, nidhamu na viwango vya utendaji vinavyotakiwa katika utumishi wa umma.
“Taswira na heshima ya NPS kwa umma na taasisi nyingine inajengwa kupitia utendaji, mienendo mizuri, hivyo ni wajibu wenu kuwa mfano bora kwa watumishi mnaowaongoza na kwa taasisi kwa ujumla”
Aidha, amewataka viongozi hao kuhakikisha maazimio yote yaliyotolewa katika Mkutano Mkuu wa UTATU yanatekelezwa kikamilifu, kuendelea kusimamia vikao vya weledi, kuimarisha ushirikiano wa taasisi zinazounda umoja huo na kuzingatia umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa mashauri pamoja na kuhakikisha taarifa zote za kesi zinaingizwa kwenye mfumo kwa wakati.
DPP Mwakitalu alisisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kuhakikisha mashauri yanaendeshwa na kumalizika kwa wakati, kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na weledi, huku wakifuatilia kwa karibu utendaji wa watumishi walio chini yao ili kuimarisha utoaji wa huduma bora za mashtaka kwa wananchi.
