TULINDE HAKI NA MASLAHI YA WATOTO KWENYE MFUMO WA HAKI JINAI
Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester A. Mwakitalu, amesema ni wajibu wa wadau wa haki jinai kuhakikisha watoto wanaoingia katika mfumo wa haki jinai, iwe kwa kuathiriwa na uhalifu, shahidi au kwa kutenda uhalifu wanapata ulinzi unaostahili, wanasikilizwa na kushughulikiwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na maslahi yao, bila kupoteza matumaini ya maisha yao ya baadaye ili kuwajengea mazingira yatakayowawezesha kuwa raia wema na wazalendo watakaolinda na kujenga taifa.
Bw. Mwakitalu amebainisha hayo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Taarifa ya Ukaguzi wa Watoto Wanaokinzana na Sheria waliopo katika Vizuizi uliofanyika tarehe 22 Septemba, 2026 Jijini Dodoma. Hafla hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa Taratibu za Uendeshaji wa Mashauri ya Watoto. Ameongeza kuwa uzinduzi wa taarifa pamoja na miongozo hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa haki jinai unaozingatia haki, utu na maslahi ya mtoto.
Amesema ukaguzi uliofanyika ulilenga kubaini changamoto zilizopo katika mifumo ya kushughulikia watoto wanaokinzana na sheria, ikiwemo changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya vizuizi na wakati wa uendeshaji wa mashauri yao, ili kuwezesha wadau kuchukua hatua za kuboresha mifumo hiyo na kurekebisha maeneo yanayoweza kuathiri ustawi na haki za watoto.
“Ukaguzi ulifanyika katika sehemu kubwa ya vizuizi ambapo tulipita katika vizuizi 75 katika mikoa yote nchini na kuwafikia watoto wengi tuliowakuta katika vituo hivyo kwa makosa mbalimbali. Kila mtoto alikuwa na historia yake na sababu zilizomfikisha hapo alipo, hivyo taarifa hizi zitusaidie kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.” Amesema Bw. Mwakitalu.
Aidha, amesema maandalizi ya miongozo hiyo ni miongoni mwa hatua zinazolenga kupunguza changamoto katika ushughulikiaji wa mashauri ya watoto na kuhakikisha taratibu zinazotumika zinakuwa na mwelekeo unaofanana katika kushughulikia masuala yote yanayowahusu watoto wanaoingia katika mfumo wa utoaji haki.
Amewataka wadau wa haki jinai kuhakikisha miongozo hiyo haibaki kuwa nyaraka katika ofisi zao, bali inatumika katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku, huku kila mmoja akijifunza, kuitekeleza na kutoa elimu kwa wengine kuhusu umuhimu wa kuwalinda na kuwasaidia watoto wanaokinzana na sheria ili waweb raia wema.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Bi. Victoria Mgonela ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa juhudi na dhamira thabiti za kuimarisha mfumo wa haki kwa watoto nchini. Amesema taarifa hiyo ni muhimu kwa kuwa imefanyika baada ya ukaguzi wa vituo na vizuizi vinavyohifadhi watoto nchini na hivyo kutoa ushahidi muhimu kuhusu hali na mazingira ya watoto walioko mahabusu, huku ikibainisha pia mifano ya mafanikio pamoja na maeneo yanayohitaji hatua za haraka.
Aidha, amesema UNICEF ipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa watoto nchini, ili kuhakikisha watoto wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria na viwango vya kimataifa, kikanda na kitaifa. Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha mfumo wa haki jinai unazingatia maslahi na haki za mtoto.
