Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

SERIKALI YAMFUTIA KESI MWANANCHI ALIYELALAMIKA KUBAMBIKIZIWA KESI NA POLISI
28 Aug, 2019
SERIKALI YAMFUTIA KESI MWANANCHI ALIYELALAMIKA KUBAMBIKIZIWA KESI NA POLISI

SERIKALI YAMFUTIA KESI MWANANCHI ALIYELALAMIKA KUBAMBIKIZIWA KESI NA POLISI
Serikali imemfutia kesi mwananchi Musa Adam Sadick aliyelalamika kubambikiziwa kesi ya mauaji na Polisi mkoani Tabora na kuchukuliwa pesa na simu alivyokuwa navyo wakati anakamatwa mjini Tabora.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga amesema uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya ofisi ya Taifa ya Mashtaka nchini (NPS) kuagizwa kuchunguza suala hilo ili kubaini ukweli wake kufuatia barua ya wazi aliyoandika mwananchi huyo kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kuchapishwa na gazeti la Majira Machi sita mwaka huu.
DPP Mganga amesema NPS ilifuatilia suala hilo kwa kufanya mahojiano na mlalamikaji na kuangalia nyaraka za polisi na hati ya mashtaka ambazo zilionyesha vitu tofauti na makosa aliyokuwa akishtakiwa nayo na kutokana na hali hiyo amemfutia kesi hiyo na Mahakama imemuachia huru na kuongeza kuwa Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi mkoani Tabora kuhakikisha mwananchi huyo anarudishiwa vitu vyake.
“Tumelifuatilia suala hilo, tumehojiana na mtuhumiwa, tumeangalia kitabu cha kuzuia wahalifu na hati ya mashtaka, tumegundua kuwa ni kweli mwananchi huyo alibambikiziwa kesi kwani kitabu kinaonyesha alikamatwa kwa kosa la kuvunja na kuiba na hati ya mashtaka inaonyesha anashtakiwa kwa mauaji ya Jackson Thomas, kutokana na hali hiyo nimemfutia kesi hiyo na Mahakama ya Mkoa wa Tabora imemuachia huru,” alisema DPP Mganga.
Amesema kutokana na kitendo hicho cha utovu wa nidhamu na ambacho kinachafua taswira ya Ofisi yake amemvua madaraka ya uendeshaji kesi ambayo alimkasimu askari husika na kuongeza kwamba hatosita kuchukua hatua kama hizo kwa afisa yeyote aliyemkasimu kuendesha mashtaka kwa niaba yake.
Aidha amesema Mhe. Rais ameziagiza mamlaka za nidhamu za askari huyo kumchukulia hatua stahili ili iwe fundisho kwa askari wengine wote wenye tabia kama hizo ambazo zinachafua taswira ya jeshi la polisi na serikali kw aujumla mbele ya wananchi wake.
Mhe. Rais pia amempongeza bw. Musa Adam Sadick kwa ujasiri aliouonesha wa kuweka wazi malalamiko yake ambayo yamesaidia kupata haki yake n aamelipongeza Gazeti la Majira kwa kuchapisha barua hiyo ya mwananchi na hivyo kusaidia kupata haki yake.
Machi sita, 2018 Gazeti la Majira lilichapisha barua ya wazi kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo mwananchi huyo Bw. Musa Adam Sadick alilalamika kubambikiziwa kesi ya mauaji na polisi wakati hahusiki na tuhuma hizo na kwamba yuko gereza Kuu la Tabora kutokana na tuhuma hizo ambazo si za kweli dhidi yake kwake