SERIKALI YAKABIDHIWA MALI NA FEDHA ZILIZOTAIFISHWA KUTOKANA NA UHALIFU NCHINI

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) imeikabidhi Serikali mali na fedha zinazohusiana na uhalifu ambazo zimetaifishwa kwa amri ya Mahakama.
NPS pia imekabidhi fedha zilizolipwa kutokana na kesi za madini zilizopo katika akaunti ya AFR ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zenye thamani ya Tsh Bilioni 58.6. Makabidhiano ya fedha na mali hizo zilizotokana na uhalifu yamefanyika February 10, 2020 jijini Dar Es Salaam baina ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Katibu Mkuu Hazina kwa niaba ya Serikali.
DPP Mganga amesema Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wametaifisha nyumba 24, magari 65, viwanja Tisa, mashamba mawili, mbao 6894, jahazi moja iliyokuwa ikitumika kufanya uvuvi haramu kwenye ukanda wa bahari kuu na boti moja iliyohusika katika kuingiza nchini vipodozi vyenye sumu.
‘’Hapa nakabidhi fedha zilizomo kwenye akaunti ya Asset Forfeiture Recovery (AFR) ya BOT ambazo ni Shilingi 19,639,782,781.46 ukijumuisha thamani ya madini yote, fedha iliyolipwa kutokana na kesi zinazohusiana na madini jumla yake inakuwa Shilingi billioni 58,604,375,783.56’’ alisema DPP Mganga.
Amesema tangu kuzinduliwa rasmi kwa NPS mwezi Agosti mwaka 2018, Ofisi yake imefanikiwa kutaifisha jumla ya kilo 397.937 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 32.2 zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi na kuisababishia serikali kukosa mapato na kuongeza kuwa mpaka sasa kilo 351.76 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 29 zimekabidhiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambaye ndiye mtunzaji wa mali za Serikali.
‘’Leo hii nakabidhi kilo 46.177 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 3.2, pia tumetaifisha madini aina ya Almasi, Tanzanite, Silver, Amethyst, Rhodolite, Bati, Blue Sapphire, Spinel, Ruby, Tourmaline, Acuamarine na kufanya thamani ya madini yote yaliyotaifishwa pamoja na faini zilizolipwa na washitakiwa kuwa Shilingi Bilioni 42.2’’ alisema.
Amesema kufuatia marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 11 ya mwaka 2019, Ofisi yake imeendesha kesi katika zoezi la washtakiwa kukiri makosa yao ambapo jumla ya Tsh Bilioni 12.3 zimeshalipwa kama kodi iliyokwepwa, faini na fidia katika akaunti maalum iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.
Akifafanua zaidi DPP Mganga alisema zoezi la urejeshaji wa fedha kwa washitakiwa 341 ambao hawajamaliza kutimiza makubalino linaendelea na makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa kama yalivyosajiliwa kwa amri ya Mahakama, ambapo katika madai hayo Serikali inawadai washitakiwa wote kiasi cha Shilingi Bilioni 32.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema wakati umefika kwa Watanzania kunufaika kikamilifu na uwepo na rasilimali zao ikiwemo madini ambayo katika miaka ya nyuma hayakuwa na usimamizi madhubuti, hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa yanaleta manufaa endelevu kwa wananchi wake.
Kwa upande wake Waziri wa Madini, Mhe. Dotto Biteko amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuzingatia sheria kwa kuwa serikali haitokuwa na msamaha kwa mtu yoyote atakayejihusisha na vitendo vya utoroshaji wa rasimali madini nje ya nchi kwani yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuinyima nchi mapato.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema zoezi la utaifishaji wa mali za uhalifu, ni ishara kuwa Tanzania sio nchi maskini na hivyo hakuna sababu ya Serikali kwenda kukopa nje ya nchi na badala yake itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa raslimali zake zitalindwa kwa nguvu zote.