SERIKALI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KINGONO KWA WATOTO
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainab Katimba amesema kwamba serikali ya awamu ya sita itaendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kingono kwa watoto na usafirishaji haramu wa binadamu kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na haki zao zinalindwa ili kujenga taifa imara.
Akizungumza leo Februari 23, 2026 jijini Dar es Salaam, Mhe. Katimba, amesema serikali itaendeleza juhudi hizo kupitia ushirikiano wa taasisi mbalimbali za haki jinai ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na wadau wengine wa maendeleo.
Mhe. Katimba ametoa kauli hiyo alipotembelea Kikosi Kazi cha Ulinzi wa Mtoto dhidi ya Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu (AHTCP-TF), kwa lengo la kujionea namna kikosi hicho kinavyotekeleza majukumu yake. Alipongeza kazi inayofanywa na kikosi hicho kwa kushirikiana na wadau wengine katika kufichua na kuvunja mitandao ya kihalifu inayohusisha ukatili wa kingono kwa watoto na usafirishaji haramu wa binadamu.
“Hii kazi imeonyesha matokeo makubwa kwa mitandao ya usafirishaji haramu wa binadamu iliyokuwepo kukamatwa na kuwasaidia wahanga kurudi katika jamii zao,” amesema Mhe. Katimba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Divisheni ya Utaifishaji Mali, Makosa yanayovuka Mipaka na Uhalifu Mahsusi (DAFT) kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), ambaye pia ni msimamizi wa Kikosi Kazi, Faraja Nchimbi, ameeleza kuwa Kikosi Kazi hicho hakikuundwa kwa lengo la kuchukua au kuingilia majukumu ya vyombo vya uchunguzi, bali kimeanzishwa mahsusi ili kuunda timu ya wataalamu waliobobea katika masuala ya ulinzi na ustawi wa mtoto.
Amefafanua kuwa lengo kuu la kikosi hicho ni kuchunguza na kuvunja mitandao mikubwa ya kihalifu, hususani inayojihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na makosa ya unyanyasaji wa kingono, ili kung’oa kabisa mizizi ya uhalifu wa aina hiyo na kuimarisha usalama wa watoto katika jamii.
Naye Mkuu wa Kikosi Kazi cha Ulinzi wa Mtoto Dhidi ya Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu, SACP Tulibake Kasongwa, amesema kuwa katika operesheni mbalimbali zilizofanyika, manusura 233 wameokolewa na kupatiwa huduma za kisaikolojia, kiafya na kijamii ili kuwawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Ikumbukwe kuwa Kikosi Kazi hicho kilianzishwa mwaka 2022 na Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 4A cha Sheria ya Huduma za Mashtaka, kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, kwa lengo la kuratibu na kuharakisha upelelezi, uendeshaji wa mashtaka pamoja na kuhakikisha manusura wanapatiwa ulinzi na msaada unaostahili katika mchakato mzima wa haki.
