TUGHE TAWI LA NPS YAFANYA UCHAGUZI WA VIONGOZI
Watumishi ambao ni wanachama cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Tanzania (TUGHE) Tawi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wamefanya uchaguzi wa viongozi wapya wa Tawi hilo watakao hudumu kwa kipindi cha 2026 – 2031.
Uchaguzi huo umefanyika tarehe 27 Machi, 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma ambapo walipatikana viongozi katika nafasi mbalimbali kwa mujibu wa katiba ya TUGHE inayotaka kuwapo kwa viongozi wa nafasi mbalimbali ndani ya chama.
Akizungumza wakati akifungua mkutano ulioambatana na uchaguzi wa viongozi wa TUGHE Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema uwepo wa vyama vya wafanyakazi ni muhimu sana kwa ustawi wa wafanyakazi pamoja na taasisi hivyo amewataka wanachama wao kufanya uchaguzi kwa kuzingatia misingi ya haki, demokrasia na uwazi ili kuweza kupata viongozi wenye sifa, uwezo wa kuongoza na ambao wapo tayari kutumikia chama na watumishi kwa kujituma.
“Mnafahamu ofisi yetu imebeba jukumu kubwa la kusimamia mashtaka hapa nchini jambo ambalo linagusa haki za watu hivyo ili kuweza kutekeleza jukumu hilo kwa ukamilifu tunahitaji kuwa na wafanyakazi waadilifu, wawajibikaji na wenye weledi.” Amesema DPP
Aidha amewataka viongozi watakaochaguliwa kwenda kuwahimiza watumishi ambao wanasifa za kuwa wanachama kujiunga na chama hicho ili kuimarisha chama na pia kuweza kutekeleza majukumu yao kwa umahili Zaidi.
“Ni matarajio yangu katika mkutano huu mtajadili na kupata nafasi ya kuzungumza mambo yote yanayowahusu ninyi kama wafanyakazi na yanayohusu taasisi yetu na utendaji kazi wake pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kukumbusha wajibu wa kufanya kazi ndani ya taasisi yetu.” Amesema Mkurugenzi Mwakitalu
Pia amewashukuru viongozi wa chama pamoja na Menejimenti ya NPS kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa kwa lengo la kuimarisha maslahi ya watumishi pamoja na mazingira ya kazi.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, alimpongeza Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na Menejimenti ya NPS kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha chama kinaendelea kuwa na tija kwa watumishi na taasisi kwa ujumla. Alibainisha kuwa ushirikiano uliopo umechangia kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi.
“Chama hiki kimefanikiwa kuimarisha mshikamano wa watumishi kwa kushirikiana na Menejimenti. Tunashuhudia ongezeko la ushiriki wa watumishi katika shughuli mbalimbali za kijamii, kitaifa na hata nyakati za dharura kama vile misiba.” Amesema Bi. Kileo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuleta chachu mpya ya uongozi, kuimarisha ustawi wa watumishi na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
