OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YASHIRIKI KIKAO CHA 61 CHA BARAZA LA HAKI ZA BINADAMU – GENEVA, USWISI
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa haki za binadamu, imeshiriki Kikao cha 61 cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu kinachoendelea kufanyika jijini Geneva, Uswisi, kuanzia tarehe 23 Februari hadi 03 Aprili, 2026.
Lengo kuu la kushiriki kikao hicho ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kulinda na kukuza haki za binadamu, kubadilishana uzoefu na mbinu bora katika utekelezaji wa haki za binadamu, pamoja na kuwasilisha hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025 katika kulinda na kukuza haki za binadamu na utawala wa sheria.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulijumuisha Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi zake na wadau wengine wa haki jinai. Kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, ujumbe uliwakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa Dhidi ya Binadamu na Utangamano wa Taifa Bw. Renatus Mkude na Wakili wa Serikali Mwandamizi Bw. Juma Mahona.
Katika kikao hicho, nchi wanachama zimejadili masuala mbalimbali ya haki za binadamu, ikiwemo usikilizwaji kwa haki (fair trial), mapambano dhidi ya vitendo vya mateso (torture), ukatili wa kijinsia (GBV), adhabu ya kifo, pamoja na ulinzi wa haki za watoto hususan katika mazingira ya migogoro ya silaha.
Aidha, ujumbe wa Tanzania ulilihakikishia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda na kuheshimu haki za binadamu kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa. Ujumbe huo pia uliwasilisha hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kushughulikia matukio ya kijinai yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ikiwemo uamuzi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi kuchunguza matukio hayo.
