Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

OFISI ZA MASHTAKA WILAYA KUENDELEA KUIMARISHWA - DPP
06 Apr, 2023
OFISI ZA MASHTAKA WILAYA KUENDELEA KUIMARISHWA - DPP

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inaendelea kuimarisha huduma za utoaji haki kwa wananchi ambapo katika kuboresha huduma hizo inatarajia kufungua Ofisi mpya za wilaya  50 katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kinachofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 6 Aprili, 2023 Mjini Morogoro.

Sambamba na kufungua Ofisi mpya amesema Ofisi za Mashtaka za Mikoa na Wilaya zilizokuwepo zinaendelea kuimarishwa kwa kuongeza vitendea kazi, kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza maslahi kwa watumishi pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali yakayowaongezea ufanisi katika utendaji kazi.

Amesema ili kuhakikisha utendaji kazi unaboreshwa ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 ofisi imezingatia vipaumbele vya kuimarisha utoaji wa huduma za kimashtaka kwa wananchi, kuimarisha shughuli za kuratibu Upelelezi pamoja na kufanya Ukaguzi kwenye maeneo ambayo washtakiwa au wahalifu wanatunzwa.

"Katika uimarishaji huu tumeweka kipaumbele kwenye kupata vitendea kazi vikiwepo magari, kompyuta, na printa ambavyo vitatuwezesha katika kutoa huduma bora na kwa ukamilifu kabisa kwa wananchi." Amefafanua  Mkurugenzi Mwakitalu." .

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka aliwataka Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kushiriki kikamilifu kwenye mijadala na majadiliano na pia kufikia maamuzi na maazimio ya kikao hicho cha Baraza kwa maslahi ya Watumishi, maslahi ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kwa Taifa kwa ujumla.

"Tunalo jukumu kubwa la kuwahudumia wananchi kwenye eneo hili ambalo tumekabidhiwa na ili tuweze kulitekeleza kikamilifu jukumu hili tunatakiwa kushiriki kikamilifu kwenye mijadala na majadiliano katika kikao hiki." Alisisitiza.

 Naye  Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande  akizungumza katika kikao hicho alisema katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi Menejimenti inapata nafasi ya kusikia sauti ya watumishi pamoja na kupata malalamiko na mapendekezo na mawazo ya watumishi kwa ujumla yanayosaidia katika kuboresha utendaji kazi.

Kwa upande wake Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Samwel Nyungwa ameishauri Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuhakikisha inafanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi mara mbili kwa mwaka ili   
Kutekeleza takwa la kisheria linaloloelekeza kufanyika kwa  vikao viwili kwa mwaka.

 Alifafanua kuwa kikao kimoja ni kwa ajili ya mipango na kikao cha pili ni kwa ajili ya tathmini baada ya kumaliza robo ya kwanza ya mwaka wa fedha ili kuisaidia menejimenti kufanya uboreshaji wa  mipango iliyopangwa mwanzoni.

 Naye mwakilishi wa TUGHE Taifa Bw. Nsubisi Mwasandende ameishauri Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kuzingatia uboreshaji wa maslahi ya watumishi na kuhimiza uwajibikaji kwa  kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi ili kuleta tija na  kutimiza malengo yaliyokusudiwa na ofisi.

Bw. Mwasandede ameyasema hayo wakati akitoa salamu na nasaha kutoka TUGHE Taifa.