OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YASHIRIKI PROGRAMU YA KUWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI NA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Leo tarehe 29/05/2025 Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeshiriki kikao kazi kilichohusu programu ya kuwezesha wanawake kiuchumi na kupinga ukatili wa kijinsia, kilichofanyika Jijini Dodoma.
Programu hiyo inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Amon Mpanju amesema kuwa Wizara, imelenga kuhamasisha Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kwa kuhakikisha usawa baina ya wanawake na wanaume pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili katika jamii.
Mpanju ameongeza kuwa mradi huo unajengwa kwenye misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inahimiza usawa miongoni mwa wanadamu, ambapo pia serikali ya awamu ya sita ya Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa ikihimiza juu ya ushirikishwaji wa wanawake katika sekta zote za kiuchumi huku akitoa rai kwa jamii kuachana na mila potofu zinazowabagua watoto wa kike.
Kwa upande wake Bi. Lucy Uisso Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mshtaka akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake amesema jamii imekuwa na uelewa mkubwa kuhusiana na makosa ya Ukatili wa Kijinsia tofauti na miaka ya nyuma kwani matukio mengi yameripotiwa, kufikishwa mahakamani na washtakiwa kupewa adhabu stahiki.
Amesisitiza kuwa kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, imeweka mkakati kuhakikisha kesi hizo zinasikilizwa na zinahitimishwa ndani ya muda mfupi ili kupata matokeo mazuri. Jambo lililoungwa Mkono na Mtakwimu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Alex Shayo.