Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAKABIDHI MALI ZITOKANAZO NA UHALIFU ZA SHILINGI BILIONI 4.4
04 Oct, 2022
OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAKABIDHI MALI ZITOKANAZO NA UHALIFU ZA SHILINGI BILIONI 4.4

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekabidhi Wizara ya Fedha na Mipango mali 8,188 zenye thamani ya Shilingi bilioni 4.4 zilizotokana na uhalifu

Mali hizo zilikabidhiwa Oktoba 3, 2022 na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Bw.Sylvester Mwakitalu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba.

Mali hizo zimeshikiliwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Njombe, Morogoro, Dodoma, Kagera na Dar es Salaam.

Akizungumza Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Chotto Sendo amesema makabidhiano hayo yanahusu nyumba 19, viwanja (9), mashamba mawili (2), vyombo vya moto (63), magari 31 na pikipiki (9).

Nyingine ni mbao (4,796), madumu (109) ya lita 20 kila moja ya mafuta ya ndege/taa, mashine moja ya kukobolea mpunga na madini bati yenye uzito wa kilo 2,104.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema awali baadhi ya mali walizokabidhi Serikalini siku za nyuma, zilileta changamoto kwa washtakiwa kukataa rufaa na mahakama kutengua maamuzi ya mwanzo.

Amesema hiyo ndio sababu kuu ya mali hizo kuendelea kushikiliwa na ofisi yake kwa kipindi hicho ili kutoa nafasi kwa washtakiwa kutafuta haki zao zote kabla ya kuzikabidhi kwa Serikali.

Amesema kuwa mali wanazokabidhi leo hazina kipingamizi kwasababu washtakiwa walipata nafasi ya kutafuta haki zao hadi mahakama za juu ama wengine waliridhika na uamuzi wa mahakama.

“Kwa mujibu wa sheria zetu mhalifu hatakiwi kunufaika na mali alizopata kutokana na uhalifu. Kwasababu zikibaki kwa wahalifu zitatumika kufadhili uhalifu mwingine au zitawanufaisha wahalifu na kuonyesha jamii uhalifu unalipa,” aliyasema hayo Mkurugenzi wa Mashtaka.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba amesema baada ya kukabidhiwa kwa mali hizo watafanya uchambuzi kuona zinazofaa kwa ajili ya matumizi ya Serikali ambazo watazigawa kwa taasisi za umma zikaendelee kutoa huduma na zisizofaa kwa matumizi ya Serikali zitapigwa mnada.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka aliwataka wahalifu kuacha kutenda uhalifu kwakuwa haulipi