OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA NI JESHI LA KULINDA NCHI DHIDI YA UHALIFU WOWOTE, NDANI NA NJE YA MIPAKA YA NCHI.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni jeshi la kulinda nchi dhidi ya Uhalifu wowote, ndani na nje ya mipaka ya nchi na sifa kubwa ya Jeshi ni kushiriki mapigano ili kuiweka nchi na jamii kuwa salama.
‘’Kazi yenu ninyi ni kuhakikisha katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunakuwa na haki, Amani, usawa, na maendeleo. Tukikosa haki na usawa tutakosa amani na nchi haitatawalika, kwa sababu wahalifu hawatakuwa na wasiwasi tena.”
Waziri Ndumbaro ameyasema hayo katika hafla ya kukabidhi magari 16 yaliyonunuliwa na Serikali kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kutumika kwenye ofisi za wilaya zake 16 iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2025 katika jengo jipya la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka lililopo Njedengwa, mtaa wa Mashtaka Jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo Bw. Ndumbaro alisema kuwa magari yaliyokabidhiwa ni utekelezaji wa moja ya Ilani ya chama cha mapinduzi 2020-2025 ya kupeleka huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za kimashtaka ambazo zinahitaji vitendea kazi kama magari.
"Mhe. Rais ameweka fedha nyingi katika maboresho ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, tunaona jengo la ghorofa saba ambalo linakaribia kukamilika, magari mapya ya ziro kilomita na uwezeshaji unaofanyika katika ofisi za mikoa na wilaya, pia Mh. Raisi ameleta ajira nyingi katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashauri.” Amesema Dkt. Ndumbaro.
Pia amewahimiza Wakuu wa Mashtaka wa Wilaya na Madereva wanaokwenda kukabidhiwa magari hayo kuyatunza, kuyatumia na kuyaendesha kwa umakini kwani ni magari ya umma na hivyo yatumike kwa shughuli za umma na serikali ili yarahisishe utekelezaji wa majukumu ya kila siku jambo litakalosaidia kupata vitendea kazi zaidi.
Aidha, Mhe. Ndumbaro ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka chini ya Uongozi wa Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu na Menejimenti yake kwa kujenga timu imara inayofanya kazi vizuri na kupelekea malalamiko ya kesi kupungua.
Amesisitiza kuwa kazi ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni kulinda nchi dhidi ya uhalifu, sio kuonea mtu bali kumfikisha mhalifu pale anapostahili, kwenda jela iwapo ana hatia au kuachiliwa huru iwapo hana hatia kupitia mhimili wa mahakama.
Sambamba na hilo Waziri Ndumbaro ametoa wito kwa Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha nchi inakuwa na amani na usalama huku wakishughulika na ukatili wa kijinisia, utapeli katika masuala ya ardhi na kughushi nyaraka katika mambo ya mirathi ambayo ni masuala yaliyobainika katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia na kuihimiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria kwa uhalifu utakaotendeka katika kipindi hiki cha uchaguzi kwani sheria hazeindi likizo.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kuipatia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka magari ambayo ni vitendea kazi muhimu katika kutekeleza jukumu lake kuu la kuratibu upelelezi na uendeshaji wa Mashtaka.
Pia ameeleza kuwa ugawaji wa magari hayo katika wilaya 16 zenye ofisi ya mashtaka umezingatia umbali na uhitaji wa kila wilaya ambapo magari hayo yatarahisisha utembeleaji wa vituo vya polisi na magereza kuwaona wazuiwa.
Aidha magari hayo yamegaiwa katika wilaya za Momba, Kilosa, Gairo, Kilombero, Buhigwe, Iramba, Misenyi, Nyangh’wale, Ubungo, Kyera, Kilwa, Kaliua, Muleba, Uvinza na Kilolo ambayo yataongeza kasi ya utendaji kazi hususan uratibu wa upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.