Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekuwa msaada mkubwa kwa TRA” – Mkurugenzi Shigela
23 Jan, 2025
“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekuwa msaada mkubwa kwa TRA” – Mkurugenzi Shigela

Mkurugenzi wa Sheria kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Elisha Shigela akimwakilisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  imekuwa msaada mkubwa katika suala zima la ushughulikiaji wa mashauri yanayohusiana na ukwepaji wa kodi.

“Ukiangalia sehemu kubwa ya kodi inayokusanywa inatokana na ule ulipaji kodi wa hiari (voluntary compliance) na mara nyingi kuna watu ambao wameamua kutokulipa kodi hivyo tunaamua kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria na ndipo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inapokuja kuungana na TRA kufanya upelelezi wa kina na kugundua makosa yanayofanywa na watu husika na baada ya kukamilisha upelelezi tunawapeleka mahakamani wahusika hao na kuhakikisha kwamba tunakomesha tabia ya kutokulipa kodi”.

Mkurugenzi wa Sheria amebainisha hayo wakati alipotembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 17 Januari, 2025 akiwa ameambatana na timu yake kutoka Makao Makuu ya TRA Jijini Dar es salaam kwa lengo la  kuwashukuru wakiwa kama wadau wao katika shughuli za ukusanyaji wa kodi kwani wamekuwa msaada mkubwa sana katika masuala hayo.

Aidha, Mkurugenzi Shigela amesema wataendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na ikiwezekana kuwepo na dawati litakalowezeshwa kushughulikia makosa yanayotokana na kodi na katika hilo TRA watakuwa tayari kuandaa  programu  ambazo watawawezesha Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kupatiwa mafunzo ya pamoja.

“Ili kuweza kufanya kazi vizuri katika eneo fulani lazima uwe unalifahamu vizuri pamoja na umahiri wa kutosha, hivyo tungependa kuwahusisha katika mafunzo mbalimbali yanayofanywa na TRA ili waweze kuwa na umahiri katika kujua kodi yenyewe na kujua namna ya kuweza kushughulikia makosa yatokanayo na kodi.” Amefafanua Mkurugenzi Shigela.

Kwa upande wake Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi kodi Bi. Feliciana Nkane ameiomba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendeleza ushirikiano wa pamoja katika kudhibiti masuala yanayohusiana na makosa ya kodi kwa kuwapeleka watu mahakamani ili kutuma ujumbe kwa wengine ambao wanakwepa kodi ili kuweza kufahamu kwamba ukwepaji kodi ni kosa la jinai na unaweza kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Sisi sote ni Watoto wa baba mmoja na tunajenga nyumba moja hivyo tunachoomba kutoka kwenu ni ushirikiano hususani katika masuala ya Upelelezi wa makosa yanayohusiana na kodi.

Rai yangu tunahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwenu kwani ninyi ndio wataalamu zaidi katika maeneo haya na msichoke kutuongoza na kutupa miongozo mbalimbali kuhakikisha kwamba tunatengeneza kesi zilizo bora”. Amebainisha hayo Naibu Kamishna.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema ujio wa TRA  katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni muhimu sana kwasababu unawafungulia njia (platform) ya kuweza kushirikiana zaidi na pia kutafuta namna ambayo wakiamua kwenda mahakamani wanaenda wakiwa na uhakika wa kushinda mashauri kwa asilimia kubwa.

“Niwaombe kupitia platfom hii tushirikiane kuanzia tunapoliandaa jalada, tunapokusanya ushahidi na tunapokwenda mahakamani hizi timu za Wapelelezi na Waendesha Mashtaka kutoka pande zote ziwe zinashirikiana.” Amesisitiza Mkurugenzi Mwakitalu.

Mkurugenzi Mwakitalu ameishukuru pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwapatia fursa ya mafunzo kwani bila kujenga uwezo wa watendaji nafasi ya mafanikio inakuwa ndogo na hafifu. Aidha ameomba mafunzo yatakayofanyika kwa ufadhili wao,yashirikishe pia wadau wetu muhimu hasa vyombo vya upelelezi ili wanapofanya chunguzi hata za makosa mengine, wasiache pia kuchunguza makosa ya kodi yanayobainika kwa sababau tu ya kukosa maarifa ya kutosha juu ya eneo hili.