NPS YAWANOA MAWAKILI UENDESHAJI WA MASHAURI YA WATOTO
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) imeendesha mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kuhusu uendeshaji wa mashauri ya watoto wanaokinzana na sheria, kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazosimamia mashauri hayo, pamoja na kuboresha namna ya kuyashughulikia.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 23 Septemba, 2026 mkoani Morogoro, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, amesema NPS imeona umuhimu wa kuwajengea uwezo Mawakili hao kufuatia uzinduzi wa Taarifa ya Ukaguzi wa watoto wanaokinzana na sheria pamoja na Taratibu za Uendeshaji wa Mashauri ya Watoto, ili kubaini changamoto na kuweka hatua za pamoja za kuzitatua.
Amesema kuwa kuwepo kwa miongozo ya pamoja kutasaidia kuhakikisha mashauri ya watoto yanaendeshwa kwa viwango vinavyofanana katika mikoa yote, huku Tanzania ikiendelea kuheshimu sheria na mikataba ya kikanda na kimataifa inayolenga kulinda haki na maslahi ya mtoto.
Bi. Kileo amesisitiza kuwa NPS ina jukumu kubwa la kulinda haki na usalama wa watoto, hivyo katika kushughulikia mashauri yao ni muhimu kuzingatia mazingira na mahitaji maalum ya kila mtoto, kwa lengo la kumsaidia kujirekebisha na kuwa raia mwema baada ya kumaliza taratibu au adhabu inayostahili.
Aidha, amewataka Mawakili hao kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kubadilishana uzoefu na kuongeza umahiri, huku wakizingatia maslahi bora ya mtoto katika kila hatua ya shauri. Amesema watoto wanapaswa kushughulikiwa kwa namna inayolinda haki, usalama na utu wao, iwe ni watoto wanaokinzana na sheria, shahidi au walioathirika na makossa ya uhalifu.
Kwa upande wake, Mtaalam wa Ulinzi wa Watoto kutoka UNICEF Bi. Victoria Mgonela amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kuimarisha maarifa na kujenga dhamira ya pamoja katika uendeshaji wa mashtaka unaozingatia haki na mahitaji ya watoto. Aidha, amesisitiza kuwa watoto wanahitaji sio tu mchakato wa kisheria bali wanahitaji ulinzi, uelewa na fursa ya kurekebishwa na kurejea katika jamii wakiwa raia wema.
Amehimiza washiriki kushirikiana kikamilifu na kutumia maarifa waliyoyapata katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ili kuhakikisha watoto wanatendewa kwa haki na maslahi yao yanalindwa.
