Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

NPS YASHIRIKI UFUNGUZI WA MICHEZO YA 40 YA SHIMIWI
20 Nov, 2026
NPS YASHIRIKI UFUNGUZI WA MICHEZO YA 40 YA SHIMIWI

Mashtaka Sports Club ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ikiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, pamoja na Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Jukael Jairo, imeshiriki katika ufunguzi rasmi wa Mashindano ya 40 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).

Ufunguzi wa mashindano hayo umefanyika Septemba 27, 2026 Moshi, Mkoani Kilimanjaro, chini ya kauli mbiu “Watumishi wa Umma Tuko Tayari AFCON 2027.” Huku Mgeni Rasmi akiwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda (Mb).

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Makonda amesema michezo ina umuhimu mkubwa kwa watumishi wa umma, si katika kuimarisha afya pekee, bali pia katika kujenga umoja, ushirikiano, uzalendo na mshikamano miongoni mwa watumishi.

Amesema michezo hiyo pia inatoa fursa kwa watumishi kutoka taasisi na maeneo mbalimbali nchini kukutana, kushirikiana na kujenga mahusiano mazuri yanayo changia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, Mhe. Makonda ameomba mashindano yajayo kufanyika katika Mkoa wa Arusha, huku akihimiza kuongezwa kwa thamani ya mashindano hayo kupitia uimarishaji wa motisha na zawadi kwa washiriki, hususan zawadi za fedha taslimu.

Mashtaka Sports Club inaendelea kushiriki katika michezo mbalimbali ya SHIMIWI 2026, ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, kuvuta kamba, mbio za baiskeli, kurusha tufe pamoja na michezo mbalimbali ya jadi.