NPS YASHIRIKI SEMINA YA WAAJIRI NA VIONGOZI WA TUGHE
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, ameshiriki Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), inayolenga kuimarisha mahusiano baina ya waajiri na watumishi, kuboresha utendaji kazi na ustawi wa wafanyakazi katika taasisi za umma.
Semina hiyo ya siku tano inafanyika kuanzia Novemba 9 hadi 13, 2026, katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha, ikiwakutanisha waajiri na viongozi wa TUGHE kutoka Wizara, Taasisi na Ofisi za Umma nchini. Bi. Kileo ameambatana na viongozi wa Divisheni ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala pamoja na Mwenyekiti na Wajumbe wa Halmashauri ya TUGHE Tawi la NPS.
Akizungumza na viongozi wa TUGHE Tawi la NPS walioshiriki semina hiyo, Bi. Kileo amewapongeza kwa juhudi zao za kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi na kuwa kiungo muhimu kati ya watumishi na Menejimenti ya Ofisi. Aidha, amewahimiza kutumia maarifa watakayoyapata katika semina hiyo kuboresha utendaji na ustawi wa watumishi.
“Elimu hii mtakayoipata hapa, mkaitumie vema kwanza kwa kuwaelimisha wale ambao hawakushiriki semina hii na pili kuwashauri viongozi wa taasisi yale yote yanayohitajika kwa ajili ya kuleta tija katika utendaji kazi na ustawi wa taasisi,” amehitimisha Bi. Kileo.
