Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

NPS YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA MWAKA WA TBPA ARUSHA
16 Jul, 2026
NPS YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA MWAKA WA TBPA ARUSHA

Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, wameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TBPA), uliofanyika Julai 13, 2026, jijini Arusha.

Mkutano huo wa siku mbili wenye kaulimbiu "Haki, Wajibu na Utawala wa Sheria ni Msingi wa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050" umefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika hotuba yake, Rais amewataka Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi, maadili ya taaluma na sheria, huku wakilinda maslahi ya Taifa.

Aidha, Rais Dkt. Samia amepongeza taasisi za sekta ya sheria zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, ikiwemo NPS, kwa huduma wanazozitoa kwa wananchi na mchango wao katika kuimarisha utoaji haki.

"Nimetembelea mabanda ya taasisi za sekta ya sheria na nimeona huduma mbalimbali mnazozitoa pamoja na kazi nzuri mnazofanya katika usimamizi na utekelezaji wa sheria. Nimeona malengo na mipango yenu. Hongereni sana. Serikali ipo pamoja nanyi, na tutahakikisha mnafikia malengo yenu," amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.