NPS YAPATA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma, imepata mafunzo ya kukabiliana na dharura na majanga ya moto yaliyotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, yenye lengo la kuwajengea watumishi uelewa na ujuzi wa namna ya kujikinga, kuokoa maisha na kulinda mali pindi majanga ya moto yanapotokea.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 13 Oktoba, 2026, jijini Dodoma, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwawezesha watumishi kutambua vihatarishi vinavyoweza kusababisha majanga ya moto na kufahamu hatua sahihi za kuchukua wakati wa dharura ili kujilinda wao wenyewe na kuwasaidia wengine.
Amesema kuwa usalama wa watumishi ni kipaumbele kwa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa watumishi wanapata elimu na ujuzi unaowawezesha kukabiliana na majanga mbalimbali kwa wakati. Aidha, amesisitiza kuwa pamoja na kuwepo kwa miongozo ya usalama, ni muhimu kwa kila mtumishi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kuzuia majanga na kukabiliana nayo pindi yanapotokea.
Bi. Kileo amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kufuatilia kwa umakini maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, hususan kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto na taratibu za kufuata wakati wa dharura. Ameeleza kuwa uelewa huo utawasaidia kuchukua hatua sahihi kwa haraka na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na majanga ya moto.
Aidha, amewataka washiriki kuwa mabalozi wa usalama kwa kuwashirikisha watumishi wengine maarifa watakayoyapata kupitia mafunzo hayo, ili kujenga uelewa mpana kuhusu kinga na udhibiti wa majanga ya moto katika maeneo ya kazi. Amesisitiza kuwa kila mtumishi ana wajibu wa kuzingatia kanuni za usalama na kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama kwa watu na mali.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa na tija katika kuimarisha utayari wa watumishi kukabiliana na dharura, kuokoa maisha ya watu na kulinda mali za Serikali na wananchi kwa ujumla. Aidha, ameeleza kuwa elimu hiyo itasaidia kujenga utamaduni wa kuzuia majanga kabla hayajatokea badala ya kusubiri kukabiliana na madhara yake.
