Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

NPS YAIMARISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE
20 Nov, 2026
NPS YAIMARISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE

Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) imeendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo uendeshaji wa mashtaka ya jinai, usimamizi na uratibu wa upelelezi, ukaguzi wa magereza na vituo vya polisi, pamoja na uratibu wa mashauri yanayohusiana na uhamishaji wa wahalifu ndani na nje ya nchi.

Bw. Mwakitalu ameyasema hayo Oktoba 13, 2026, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya NPS kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, alipotembelea Makao Makuu ya Ofisi hiyo kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akielezea ukuaji wa taasisi hiyo, Bw. Mwakitalu amesema chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, idadi ya watumishi wa NPS imeongezeka kutoka 630 Machi 2021 hadi kufikia 1,264 Septemba 2026, wakiwemo Mawakili wa Serikali, Makatibu Sheria na watumishi wa kada nyingine. Ongezeko hilo limechangia kuimarisha uwezo wa Ofisi katika kutekeleza majukumu yake.

Aidha, amesema NPS imekuwa ikitekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kupitia kaguzi wa magereza na vituo vya polisi. Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, Ofisi hiyo ilifanya ziara za ukaguzi katika magereza 94 kwa jumla ya mara 198 na vituo vya polisi 483 kwa jumla ya mara 931. Ukaguzi huo umesaidia kupunguza msongamano katika mahabusu na magereza nchini.

Sambamba na hayo, Bw. Mwakitalu amesema NPS imeendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kuhusu utenganishaji wa shughuli za upelelezi na mashtaka kwa kufungua ofisi za wilaya.

“Tunaendelea kusogeza huduma za mashtaka karibu na wananchi ambapo, katika mwaka wa fedha 2026/2027, ofisi sita za wilaya tayari zimefunguliwa na kuanza kazi, hatua inayofanya jumla ya ofisi za NPS kufikia 123. Uwepo wa ofisi hizi umesaidia kuhakikisha kuwa shughuli za mashtaka zinaendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,”amesema DPP Mwakitalu

Hata hivyo, Bw. Mwakitalu, kwa niaba ya watumishi wa NPS, ameahidi kumpa ushirikiano Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.