NAIBU MKURUGENZI WA MASHTAKA AZITAKA KAMATI ZA UJENZI WILAYANI KUSIMAMIA KIKAMILIFU NA KWA UZALENDO MIRADI YA UJENZI
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewataka wajumbe wa Kamati za Utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi na kamati za Ukaguzi na Mapokezi kwenda kusimamia kikamilifu miradi ya ujenzi ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kutumia vizuri mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani (Force Account) ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Kikao kazi na Mafunzo ya namna bora ya kutekeleza miradi ya ujenzi kwa kutumia mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani (Force Account) kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Wilaya 24 kilichofanyika tarehe 7 Desemba, 2024 Jijini Dodoma.
Kikao hicho kimehusisha Wajumbe wa Kamati za Ujenzi na Kamati za Ukaguzi na Mapokezi kutoka Wilaya 24, Kamati ya Uratibu wa Ujenzi Makao Makuu, Washiriki kutoka baadhi ya Divisheni na Vitengo, na Wataalamu kutoka Wakala wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Wizara ya Fedha.
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka alieleza lengo la kikao kazi hicho ni kujadiliana kwa pamoja na kupata mafunzo na miongozo ya namna bora ya kusimamia miradi ya ujenzi wa Ofisi za mikoa mitatu (3) na Wilaya 24 ambayo Ofisi imepanga kuanza kutekeleza katika mwaka huu wa fedha.
"Kwa Mwaka wa fedha 2024/2025, tumepanga kujenga Ofisi za Wilaya 24 kwa kutumia Mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani (Force account). Ofisi ilifikia uamuzi wa kutumia njia hii ili kupunguza gharama na kuwezesha kujenga ofisi nyingi zaidi hivyo, tumekusanyika ili kupata mafunzo ya Sheria, Kanuni na miongozo inayosimamia utaratibu wa ujenzi kwa njia hii lakini pia kufanya kikazi kazi kwa nia ya kupata uelewa wa pamoja ili kufanikisha lengo hili".
Aidha alifafanua kuwa Ofisi imedhamiria kwa dhati kutekeleza miradi ya ujenzi katika Mikoa na Wilaya. Aliongeza kuwa ni mkakati wa Ofisi kuendelea kuanzisha ofisi mpya na wakati huo huo kuendelea kujenga majengo ya ofisi ili kufanya kazi kwenye mazingira mazuri yatakayosaidia utoaji wa huduma bora.
"Tunawategemea sana kwenda kusimamia ujenzi wa Ofisi zetu za wilaya kwa kutumia kiasi cha pesa ambacho kimetengwa. Ni jukumu ambalo tumewapa na kuwaamini sana na pia ni jukumu ambalo litahitaji moyo wa uzalendo sana, tutambue ya kuwa fedha hiyo ni fedha ya serikali, fedha ya walipa kodi, na tumeamua kutumia njia hii ili tuweze kujenga ofisi nyingi, zenye ubora na kwa gharama nafuu, alisisitiza Naibu Mkurugenzi Bibiana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi aliwataka washiriki hao kwenda kusimamia kwa weledi mkubwa shughuli za ujenzi wa majengo ya Ofisi ya wilaya pasipo udanganyifu wa aina yoyote na wasimamie ujenzi kama wanavyosimamia mali zao binafsi kwa sababu ni fedha hizo ni mali ya Umma.
Kwa upande mwingine wataalamu kutoka Wakala wa Ununuzi wa Umma na Wizara ya Fedha walielimisha masuala mbalimbali kuhusu mfumo wa ujenzi kwa kutumia mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani ambapo washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali.