Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

NAIBU DPP ZANZIBAR AIPONGEZA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA BARA KWA MATUMIZI YA MFUMO WA TEHAMA
12 Aug, 2024
NAIBU DPP ZANZIBAR  AIPONGEZA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA BARA KWA MATUMIZI YA MFUMO WA  TEHAMA

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka kutoka Zanzibar Bi. Mwanamkaa Mohammed ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bara kwa kupiga hatua katika suala zima la matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya, Kuchakata na Kutunza Kumbukumbu za Kesi za Jinai (Case Management Information System).

Naibu DPP Zanzibar amebainisha hayo wakati wa ziara yake iliyofanyika tarehe 12 Agosti, 2024 alipotembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.

Lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kuweka mikakati katika masuala mazima yanayohusu matumizi ya Mfumo wa TEHAMA kwa kutembelea taasisi mbalimbali mbalimbali zinazohusika na masuala ya Haki Jinai na kuona wako wapi katika masuala mazima ya teknolojia, namna wanavyofanya kazi na changamoto wanazokabiliana nazo.

"Kimsingi sio CMIS tu bali ni suala zima la teknolojia  na kuona ni namna gani tunavyoitumia teknolojia kwa sababu kila tunapoenda tunaitumia teknolojia na kuachana na masuala ya karatasi, hivyo ninaamini tutaweza kupata mengi kutoka kwenu." Amebainisha hayo Naibu DPP Zanzibar.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka  Bara Bi. Bibiana Kileo ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeanza kutumia Mfumo wa CMIS mwaka 2022 na ndani ya kipindi hicho cha miaka miwili wameweza kufanya maboresho makubwa sana katika mfumo huo kwani umeweza kuwarahisishia kwenye muunganiko wa kazi zao katika ngazi ya taifa na mikoa.

"Kufuatia na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa kufikia Desemba taasisi zote ziwe zimesomana na kwa bahati nzuri sisi tumefanikiwa na katika kipindi hiki tayari tumefanikiwa mfumo wetu wa TEHAMA tayari unasomana na wadau wetu wakiwemo Mahakama, Polisi, DCI, TAKUKURU." Amefafanua hayo Naibu DPP Bibiana.