NAIBU DPP AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAAJIRIWA WAPYA
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bi. Bibiana Kileo,amekutana na kuzungumza na Waajiriwa Wapya 60 wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka kada mbalimbali (Mawakili, Madereva na Mkutubi) kwa lengo la kuwakaribisha na kufahamiana.
Waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wamewasili Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 19 Septemba, 2024 kwa lengo la kupatiwa barua zao za ajira ili kwenda kuanza kazi rasmi katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa.
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amewaasa Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu,bidii, na uzalendo mara wafikapo katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa ili kuleta chachu katika utendaji kwa ofisi na jamii yote kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi amewataka waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwenda kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia misingi ya haki pamoja na kufuata sheria na kanuni zote za utumishi wa umma.