Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Mr. Kuku ahukumiwa kulipa fidia zaidi ya sh. Bilioni 5.4
17 Dec, 2020
Mr. Kuku ahukumiwa kulipa fidia zaidi ya sh. Bilioni 5.4

Mkurugenzi wa kampuni ya Mr. kuku farmer ltd, Tariq Machibya (29), maarufu kama Mr Kuku, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kufanya biashara haramu ya upatu na kukusanya fedha za umma sh. Bilioni 17, amehukumiwa kulipa fidia ya zaidi y sh. Bilioni 5.4 baada ya kukiri mashtaka ya kushiriki katika upatu na kupokea miamala ya fedha kutoka kwa umma.

Mahakama pia imemuhukumu mshtakiwa kulipa faini ya sh. Milioni tano ama akishindwa atatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani.

Aidha mahakama imeamuru fedha sh. 5,456,480.41 ambazo zipo katika akaunti za mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya serikali.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu amesema mahakama imezingatia kwamba mshtakiwa amekiri mwenyewe makosa yake na ni mkosaji wa mara ya kwanza na wameangalia makubaliano hivyo hakuna sababu ya kumpa adhabu kali.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, amedai mshtakiwa pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) wameingia makubaliano , katika mashtaka saba aliyokuwa anakabiliwa nayo yameondolewa na wamebakisha mashtaka mawili.

Akisomewa mashtaka hayo mawili, katika shtaka la kusimamia biashara ya upatu inadaiwa kati ya Januari 2018 na Mei, mwaka huu, maeneo tofauti Dar ea Salaam alijihusisha na biashara hiyo kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma kwa kujifanya watafanya ujasiriamali wa ufugaji kuku na watapata faida asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa uwekezaji wa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kibiashara kuliko mtaji uliokusanywa.

katika shtaka la pili mshtakiwa anadaiwa kukubali kupokea muamala wa kifedha kutoka kwa umma kiasi cha Sh bilioni 17.

Awali mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka saba ambapo mbali na hayo mawili yalikuwepo mashtaka matano ya utakatishaji fedha.

Kabla ya kusomwa kwa adhabu, Wakili Kadushi aliieleza mahakama kuwa, hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya washtakiwa hivyo, ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria huku ikizingatia hatua ya makubaliano waliyofikia.

Upande wa wakili wa Utetezi, Augustine Shio ameiomba mahakama impunguzie mshtakiwa adhabu kwani amekiri makosa yake mwenyewe na pia ana familia ya wake wa watatu ambao kila mmoja anamtoto mchanga na wote wanamtegemea yeye.