MKUTANO WA JUKWAA LA HAKI JINAI TAIFA WAFANYIKA JIJINI DODOMA

Wajumbe wa Jukwaa la Haki Jinai Taifa wamekutana jijini Dodoma leo tarehe 23 Mei, 2025 kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ya maboresho ya utendaji kazi kwa Taasisi zinazosimamia Haki Jinai nchini.
Mkutano huo Jukwaa la Haki Jinai Taifa umehudhuriwa na wajumbe wa taasisi zinazounda mnyororo wa Haki Jinai nchini ambapo wamepokea pia taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, kukubaliana maazimio mapya na kuweka mpangokazi wa utekelezaji wa maazimio mapya na yale ambayo hayakutekelezwa kwa sababu mbalimbali.
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Jukwaa la Haki Jinai Taifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alisema Jukwaa la Haki Jinai limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mashtaka kifungu cha 27 ambacho kimeainisha wajumbe wanaotakiwa kushiriki kutoka katika taasisi za mnyororo wa Haki Jinai. Kifungu hicho pia kimetoa fursa ya kualika mjumbe yoyote anayeweza kusaidia katika utatuzi wa changamoto za Haki Jinai kuhudhuria katika mkutano huo ili kusaidia utatuzi wa baadhi ya masuala yanayohitaji ufumbuzi wa haraka.
Katika mkutano huo wajumbe walipata nafasi ya kupitia utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano wa Jukwaa la Haki Jinai Taifa uliopita uliofanyika jijini Dodoma.
Aidha wajumbe walipata pia nafasi ya kujua Taarifa ya Hali ya Usalama nchini, Taarifa ya Hali ya Magereza nchini, Taarifa ya Udhibiti na mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya pamoja na Taarifa ya Hali ya Usalama ndani na nje ya Hifadhi za Wanyamapori, misitu , mapori ya Akiba na mapori Tengefu.
Sambamba na hilo, wajumbe wa mkutano huo walipokea pia taarifa ya Majukwaa ya Haki Jinai ngazi ya Mikoa na Wilaya na kufanya majadiliano ya kina ya namna ya kutatua changamoto za Haki Jinai zilizoainishwa katika taarifa hiyo zinazokabili Mikoa na Wilaya zote nchini.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Taasisi zinazounda mnyororo wa Haki Jinai nchini ambao ni pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za kulevya, Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mkemia Mkuu wa Serikali, Bodi ya Parole, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori, Mamlaka ya Misitu Tanzania.