Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWANOA MAAFISA VIUNGO JUU YA NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MAKOSA DHIDI YA BINADAMU NA MAKOSA YATAKAYOJITOKEZA KATIKA KIPINDI CHA UCHAGUZI
11 Feb, 2025
MKURUGENZI WA MASHTAKA AWANOA MAAFISA VIUNGO JUU YA NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MAKOSA DHIDI YA BINADAMU NA MAKOSA YATAKAYOJITOKEZA KATIKA KIPINDI CHA UCHAGUZI

Mkurugenzi wa Mashtaka  Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kushughulikia makosa dhidi ya binadamu na yatakayojitokeza katika kipindi cha Uchaguzi mkuu ili kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa Taifa na  kuhakikisha wale wote wanaovunja sheria wanashughulika nao ipasavyo kwa kufuata taratibu na sheria za makosa ya jinai.

Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwasababu yatawakwamua katika changamoto kadhaa zinazofanya utendaji kazi wao ukwame mahali fulani na kupelekea kutokupata matokeo wanayoyatarajia.  

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mwakitalu ameipongeza Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kwa kuanzisha na kuwaita Maafisa Viungo wanaoiwakilisha  idara hiyo katika kila mkoa kwa lengo la kuwapa mafunzo.

“Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi  inasimamia asilimia kubwa ya kesi tunazoshughulika nazo huko mikoani zikiwepo kesi za Ukatili wa Kijinsia kwa maana ya Ubakaji, Ulawiti idadi yake ni kubwa sana katika Mahakama zetu, na zilizofika mahakamani ni kidogo sana ukilinganisha na matukio yanayotokea, na yale yanayoripotiwa katika Vituo vya Polisi na hayafiki asilimia 20. 
Tunayo makosa yanayogusa mali yakiwepo wizi, unyang'anyi kwa kutumia silaha, makosa haya yote yanaangukia katika idara hiyo na pia ndio makosa mengi ambayo yanafanyika kwenye jamii zetu.” Amesema Mkurugenzi Mwakitalu.

Pia Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kupitia mafunzo hayo wanatarajia kwenda kuongeza ubora wa uratibu katika Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka

“Tunategemea kuona uboreshaji zaidi juu ya namna tunavyoshughulikia Uratibu wa Upelelezi wa Makosa haya pamoja uendeshaji wake mahakamani.”

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka amewataka Maafisa Viungo hao kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kuyafahamu majukumu ya idara husika kwa ukamilifu ili kuleta mabadiliko juu ya namna ambavyo wanashughulikia makosa hayo yanayoangukia kwenye idara husika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kila baada ya mwezi mmoja ya namna wanavyotekeleza majukumu  katika mikoa yao.

Katika kuelekea kwenye kipindi cha Uchaguzi mkuu unaotarajia  kufanyika Mwezi Oktoba mwaka 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka amesema  kipindi hicho kinakuwa na mambo mengi, wananchi wana haki na wajibu wao kwenye shughuli za uchaguzi lakini wapo wale wanaopitiliza mipaka na kuvunja Sheria na kutenda makosa ya jinai,   hivyo maafisa viungo hao wanalo jukumu la kusimamia hilo Ili kudumisha amani nchini.

‘’Mtapitishwa kwenye makosa yanayohusiana na kipindi hicho na namna ambavyo tunaweza kuyashughulikia. Tunataka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tufanye kazi yetu kwa weledi hata katika kipindi hicho cha kampeni, kipindi cha maandalizi ya uchaguzi na hata baada ya matokeo ya uchaguzi, tuhakikishe tunatimiza wajibu wetu kwa Taifa, katika kuhakikisha wale wanaovunja sheria tunashughulika nao ipasavyo. Na pia pale ambapo tunaweza tukashauri makosa hayo yasifanyike basi hatuna budi kufanya hivyo.” Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza amesema kupitia mafunzo hayo Maafisa Viungo watapitishwa kwenye mada mbalimbali kuhusiana na majukumu ya idara hiyo  ambayo wanatakiwa kufanya ili kusaidia kuweza kutekeleza majukumu yao kama idara pamoja na mambo mengine. 

Aidha, watapata nafasi ya kupitishwa kwenye Ushughulikiaji wa makosa ya Ukatili wa Kijinsia.

Kama tunavyofahamu makosa ambayo yanaongoza mahakamani ni makosa ya Ukatili wa Kijinsia, tumeona tuitumie nafasi hii kuwapitisha katika  mada hiyo ili tuweze kuona ni jinsi gani makosa hayo yanaweza kushughulikiwa na changamoto zilizopo katika makosa hayo ili kuweza kuepukana na Changamoto hizo kama sio kuzipunguza basi kuziondoa kabisa.