Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Mkurugenzi wa Mashtaka atembelea gereza la Mugumu wilaya ya Serengeti
19 Aug, 2020
Mkurugenzi wa Mashtaka atembelea gereza la Mugumu wilaya ya Serengeti

Mkurugenzi wa mashtaka Bw. Biswalo Mganga hivi karibuni alitembelea gereza la Mugumu lililopo wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kukagua hali ya gereza hilo na hatimaye kufanya uamuzi wa kuwafutia kesi mahabusu themanini (80) kati yao wanaume sitini na tano (65) na wanawake (15).

Katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka aliongozana na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Serengeti.

Akizungumza wakati akiwaachia huru mahabusu hao, Bw. Biswalo Mganga aliwasihi na kuwataka mahabusu wote waliofutiwa kesi zao kwenda kuwa raia wema na kuachana na vitendo vibaya vilivyowapelekea kupelekwa katika gereza hilo.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Edson Makallo ambaye aliongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka katika ziara hiyo aliwataka mahabusu wote waliofutiwa kesi kutokurudia uhalifu kwa kuwa haulipi.

Gereza la Mugumu lina uwezo wa kuchukua jumla ya wafungwa mia mbili kumi na sita (216) lakini kutokana na ongezeko la wahalifu lilikuwa na wahalifu mia tano thelathini na mbili (532) hali iliyopelekea kuwepo kwa msongamano.