Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

MKURUGENZI WA MASHTAKA ATEMBELEA GEREZA LA ISANGA
07 Dec, 2022
MKURUGENZI WA MASHTAKA ATEMBELEA GEREZA LA ISANGA

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ametembelea Gereza Kuu la Isanga Jijini Dodoma kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili Maafisa wa Magereza katika kuwatunza wafungwa pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili mahabusu.

Akizungumza baada ya kutembelea Gereza Kuu la Isanga, Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kuwa lengo la kutembele wafungwa na mahabusu ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa misingi ya sharia na kanuni zake.

“kufanya haya yote ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo lakini tukipata hizi changamoto na kusikiliza tunaenda kuzifanyia kazi na kuzishughulikia. Changamoto tulizozipokea ambazo hazipo chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka tunazichukua na kuzipeleka ofisi ambazo zinahusika lengo ikiwa ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo.”

Amesema miongoni wa changamoto ambazo amezipokea katika ziara yake ambazo mahabusu wamezieleza ni suala zima la ucheleweshwaji wa kesi na kuchelewa kwa upelelezi ambapo ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kuzishughulikia changamoto hizo kwa kuhakikisha kuwa wameshasajili Hati za Mashtaka Mahakama Kuu ambazo hivi sasa zipo katika mchakato wa kusikilizwa.

“Mahabusu wengi ambao nimewasikiliza wamesema kesi zao zimechelewa upelelezi lakini hali halisi ni kwamba kesi zao hazijachelewa upelelezi kwa kuwa tayari umekamilika na kinachosubiriwa ni utaratibu wa kesheria ambao utawezesha kesi hizo kusikilizwa na Mahakama Kuu.”

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeanza mwendelezo wa ziara zake katika Magereza mbalimbali nchini kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili Maafisa wa Magereza, wafungwa pamoja na mahabusu ili kuhakikisha Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa mujibu wa Ibara ya 59B ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.