MKURUGENZI WA MASHTAKA AMEITAKA MENEJIMENTI NA WAKUU WA MASHTAKA WA MIKOA KUANGALIA CHANGAMOTO ZINAZOKABILI MFUMO WA HAKI JINAI NCHINI

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ameitaka Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa kuangalia changamoto zinazokabili utekelezaji wa Mfumo wa Haki jinai nchini.
"Ninyi mkiwa kama wasimamizi wa Majukwaa ya Haki jinai Mikoani lakini kwa mujibu wa majukumu yetu ninyi ni kiungo kikubwa kwenye ule mnyororo wa Haki jinai. Nafahamu mnajua mengi na mna mapendekezo mengi ambayo mnadhani yakitekelezwa Mfumo wa Haki jinai utakuwa bora. Kupitia kikao kazi hiki tutajadiliana na tutatoka na msimamo mmoja." Amezungumza Mkurugenzi Mwakitalu.
Aidha, amewataka Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa kutekeleza majukumu ya uendeshaji wa Mashtaka kikamilifu na kwa mafanikio ili kuhakikisha kesi zinasikilizwa na kuisha kwa wakati.
Bw. Mwakitalu ameyasema hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa kinachofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.
Kikao kazi hicho kimelenga katika kujadililiana na kukumbushana juu ya namna ambavyo majukumu ya Mkurugenzi wa Mashtaka yatatekelezwa kikamilifu na kwa mafanikio.
"Katika majadiliano yetu ya siku mbili tutapitia taarifa ya utendaji kazi ili kuangalia jinsi majukumu ya Mkurugenzi wa Mashtaka yanatekelezwa kwa mujibu wa Sheria, Katiba na kwa mafanikio." Amefafanua Mkurugenzi Mwakitalu."
Kikao kazi cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa kinafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Februari, 2023 Jijini Dodoma.