Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

Mkurugenzi wa Mashtaka aelezea mafanikio ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka
18 Sep, 2020
Mkurugenzi wa Mashtaka aelezea mafanikio ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka

Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Biswalo Mganga akiwa na baadhi ya Viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tarehe 17/9/2020 amefanya mazungumzo na Wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es salaam, kuelezea mafanikio ya Ofisi ya Taifa Mashtaka tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Mashtaka alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Ofisi hiyo mwaka 2018, Ofisi imefanikiwa kutaifisha baadhi ya Mali mbalimbali ambazo zilipatikana kwa njia za uhalifu zikiwemo Dhahabu, Magari, Nyumba mbalimbali na Mashamba. Mali hizo zilikabidhiwa Serikalini na kuwa mali za Serikali.

Pia na kuweza kufanikiwa kudhibiti makosa mengine ambayo yanavuka mipaka ikiwemo kesi ya madawa ya kulevya ambazo zimeendeshwa na Taasisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kuhakikisha watuhumiwa waliohusika kutenda makosa hayo wamechukuliwa hatua za kisheria.

Mkurugenzi wa Mashtaka alitoa wito kwa wadau na wananchi wote kuwasihi wale wote wanaohusika na usafirishaji wa madawa ya kulevya waache ili kuepuka kupoteza muelekeo wa maisha yao. Na kwa wale ambao wanapenda kupata Mali kwa haraka kupitia njia isiyo ya halali, mali zao zitataifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Pia Mkurugenzi wa Mashtaka alizungumzia juu ya mafanikio yakuweza kudhibiti mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ( Albino), na wote walioshiriki katika uhalifu huo walitiwa hatiani.

Bw. Biswalo Mganga alieleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka bado inazidi kuendelea kutafuta mbinu nyingine mpya za upambanaji, mojawapo ikiwepo kujenga ushirikiano na mataifa mengine ili kudhibiti makosa au uhalifu unaovuka mipaka yakiwemo madawa ya kulevya. Na hii ni kulingana na jinsi makosa mengi yanavyozidi kuongezeka kulingana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kuongezeka kwa kasi.

Mkurugenzi wa Mashtaka alimalizia kwa kuwasihi waandishi wa habari kuwakumbusha wanachi wawe wepesi wa kutoa taarifa zinazohusiana na uhalifu.