Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MKURUGENZI MSAIDIZI MKEMWA AHITIMISHA KIKAO KAZI CHA MAAFISA VIUNGANISHI
04 Dec, 2024
MKURUGENZI MSAIDIZI MKEMWA AHITIMISHA KIKAO KAZI CHA MAAFISA VIUNGANISHI

Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Udanganyifu na Utakasishaji Fedha Bw. Seth Mkemwa  amehitimisha Kikao Kazi cha Maafisa Viunganishi (Focal persons) wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili kilichofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Novemba, 2024 mkoani Morogoro.

"Katika hizi siku tatu kulikuwa na zoezi kubwa la kuchakata takwimu zinazohusiana na makosa ya Mazingira na Maliasili ambapo uchakataji wa takwimu hizi umekwenda sambamba na kubainisha changamoto, mafanikio na pia kuangalia namna ya kutafutia ufumbuzi changamoto husika”. Amebainisha hayo Bw. Mkemwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili Bw. Salimu Msemo amewapongeza Maafisa Viunganishi kwa juhudi na ushirikiano wa hali ya juu waliouonyesha katika kikao kazi hicho ikiwa ni zaidi ya vile ilivyotarajiwa.

Aidha amewataka washiriki hao kwenda kuwa watumishi wa mfano kwenye kila eneo linalohusisha majukumu yao ikiwa ni pamoja na kufuata miongozo na maelekezo yote yanayotolewa na viongozi pamoja na kuzingatia maazimio yote waliyokubaliana katika kikao kazi.

"Tutakuwa tunafanya ufuatiliaji wa hiki ambacho tumekubaliana kupitia maazimio ya kikao hiki pamoja na masuala mengine yanayohusu makosa ya Mazingira na Maliasili." Amefafanua hayo Kaimu Mkurugenzi Msemo.

Naye, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro Bi. Tarsila Gervas amewashukuru viongozi kwa kuwakutanisha Maafisa Viunganishi ili kuweza kujadili mustakabali mpana wa namna ya kupata taarifa zinazolisha taasisi katika masuala mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Bi. Neema Moshi ambae ni Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam, ameushukuru uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na wadau kwa kuwawezesha kushiriki kikao kazi hicho kwani  wamejifunza mengi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu makosa ya Mazingira na Maliasili na kuahidi kwenda kutekeleza yale yote waliyokubaliana kupitia kikao hicho.